Loliondo FM
Loliondo FM
25 August 2026, 2:40 pm

Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro imeendelea kuimarisha ushirikishwaji wa jamii katika kuzuia na kukabiliana na utapiamlo mkali kwa watoto, huku wazazi na walezi wakihimizwa kutekeleza wajibu wao katika kuhakikisha watoto wanapata lishe bora na huduma muhimu za afya.
Na mwandishi wetu.
Afisa Tarafa ya Loliondo, Bw. William Ndosi, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, ametoa rai kwa Kitengo cha Lishe kwa kushirikiana na Idara ya Maendeleo ya Jamii kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwafikia na kushirikiana na jamii katika mapambano dhidi ya utapiamlo mkali kwa watoto.
Bw. Ndosi ametoa rai hiyo Ijumaa, Agosti 14, 2026, wakati wa kikao cha Kamati ya Lishe ya Wilaya kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Amesema pamoja na jitihada zinazofanywa na Kitengo cha Lishe kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Divisheni za Afya, Mifugo, Kilimo, Elimu na Maendeleo ya Jamii katika kupunguza udumavu na utapiamlo kwa watoto, wazazi na walezi wana wajibu wa kuhakikisha watoto wanapata lishe bora na huduma stahiki za afya.
“Wazazi na walezi wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha watoto wanapata lishe bora na huduma zinazohitajika ili kuwa na afya njema,” amesema Bw. Ndosi.
Aidha, amekitaka Kitengo cha Lishe kushirikiana kwa karibu na Idara ya Maendeleo ya Jamii kuwafikia wazazi na walezi ambao hawatekelezi ipasavyo wajibu wao katika kuhakikisha watoto wanapata lishe bora na huduma muhimu.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Wilaya ya Ngorongoro, Bi. Angela Mbanga, amesema wahudumu wa afya kutoka Hospitali ya Wilaya na Hospitali ya Wasso wamepatiwa mafunzo ya utengenezaji wa maziwa maalum ya tiba, F-75 na F-100, kwa ajili ya kusaidia katika matibabu ya watoto wenye utapiamlo mkali.
Amesema maziwa hayo yana umuhimu katika kurejesha hali ya lishe kwa watoto wenye utapiamlo mkali, kwa kuwa hutengenezwa kwa kuzingatia mahitaji maalum ya virutubisho vilivyopungua mwilini, ikiwemo protini, wanga, madini, vitamini, mafuta na sukari.
Akitoa taarifa ya hali ya lishe kwa robo ya nne ya mwaka wa 2026, kuanzia Aprili hadi Juni, Bi. Mbanga amesema jumla ya watoto 61,234 walipimwa hali ya lishe katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Kati yao, watoto 60,111 (98.16%) walikuwa na hali nzuri ya lishe, watoto 1,056 (1.73%) walikuwa na hali hafifu ya lishe, huku watoto 67 (0.11%) wakibainika kuwa na hali mbaya ya lishe.
Amesema upimaji huo ulifanyika katika hospitali na vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya, ambapo Hospitali ya Wasso, Kata ya Orgosorok, ilibaini watoto 15 wenye utapiamlo mkali kati ya watoto 2,475 waliopimwa.
Katika Hospitali ya Wilaya iliyopo Lopolun, Kata ya Olorien Magaiduru, watoto 12 walibainika kuwa na utapiamlo mkali kati ya watoto 2,991 waliopimwa, huku Kata ya Alailelai ikibaini watoto 5 wenye utapiamlo mkali kati ya watoto 1,187 waliopimwa.
Hatua hizo zinaendelea kuonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, wataalamu wa sekta mbalimbali, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla katika kuzuia, kutambua mapema na kukabiliana na utapiamlo kwa watoto.