Loliondo FM
Loliondo FM
27 August 2026, 7:17 am

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro yatakiwa kuimarisha miundombinu ya barabara na maandalizi ya kukabiliana na mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza Septemba 2026.
Na Saitoti Saringe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Makala, ametoa wito kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na wilaya na taasisi nyingine za Mkoa wa Arusha, kujiandaa kukabiliana na mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza kunyesha kuanzia mwezi Septemba mwaka huu.
Mhe. Makala ametoa wito huo wakati akiongoza kikao cha Kamati ya Usalama cha Mkoa kilichofanyika katika Ofisi za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Karatu, kilichoshirikisha viongozi wa Mkoa, Wilaya za Karatu na Ngorongoro pamoja na Menejimenti ya Mamlaka hiyo.
Amesema maandalizi hayo yanapaswa kujikita katika kuhakikisha barabara, madaraja, mifereji na miundombinu mingine inakuwa katika hali nzuri ili kuepusha changamoto za usafiri, hususan katika maeneo ya utalii.
Mhe. Makala amesema Mkoa wa Arusha ni kitovu cha utalii nchini, hivyo ni muhimu kuhakikisha watalii wanaendelea kufika katika maeneo mbalimbali ya utalii bila kukumbwa na changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa.
Aidha, amesema maandalizi hayo ni muhimu pia kutokana na mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani, IPU, unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha mwezi Oktoba mwaka 2026.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Abdul-Razag Badru, amesema Mamlaka hiyo inaendelea na ujenzi wa barabara kuu kutoka Geti la Lodare hadi Golini.
Amesema kipande cha barabara chenye urefu wa kilomita 29 kutoka Lodare hadi Seneto tayari ujenzi wake umeanza, huku ukarabati wa mtandao wa barabara nyingine ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ukiendelea.