Loliondo FM

RC Makalla akemea mauaji Ngorongoro

14 September 2026, 12:17 pm

Mkuu wa mkoa wa Arusha CPA. Amos Makalla akizungumza na wananchi wa Eyasi na Kakesio. Picha na ofisi ya mkoa Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, amekemea mauaji ya wananchi wawili kutoka jamii ya Kimasai, yaliyotokea wakati wa mgogoro kati ya Wamasai na Wadatoga katika Kata za Kakesio na Eyasi, Wilaya ya Ngorongoro.

Na mwandishi wetu

Mhe. Makalla ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kuwatafuta, kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kuhusika na mauaji hayo.

Mkuu huyo wa Mkoa ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa jamii za Wamasai na Wadatoga katika Kata ya Kakesio, katika juhudi za kutafuta suluhu ya mgogoro baina ya jamii hizo mbili za wafugaji.

Mgogoro huo unahusishwa na mvutano wa matumizi ya maeneo yenye vyanzo vya maji ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Mhe. Makalla amesisitiza umuhimu wa wananchi kuheshimu sheria na taratibu za nchi, akiwataka kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ametangaza kuunda timu ya wataalamu itakayojumuisha vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wajumbe kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Sauti ya mkuu wa mkoa CPA. Amos Makalla

Timu hiyo itafanya tathmini ili kubaini chanzo cha migogoro katika eneo hilo, pamoja na kuwabaini wananchi wanaodaiwa kuvamia maeneo ya hifadhi kutoka mikoa jirani.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Justine Masejo, amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa Jeshi la Polisi limeanza kuwatafuta na kuwakamata wote watakaobainika kuhusika na mauaji hayo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Mhe. Yannick Ndoinyo, amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu kati ya jamii hizo mbili.

Mhe. Ndoinyo amewataka wananchi kushirikiana katika kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro inayohusu visima, vyanzo vya maji na maeneo ya malisho.