Loliondo FM
Loliondo FM
18 September 2026, 5:08 pm

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Brigedia Jenerali Wilson Sakulo, ameongoza kikao cha Kamati ya Maafa ya Wilaya kilicholenga kuweka mikakati ya kukabiliana na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu.
Na Saitoti Saringe
Katika kikao hicho, taasisi mbalimbali za umma, ikiwemo TANESCO, TARURA, RUWASA, Mamlaka ya Mji Mdogo wa Loliondo pamoja na Idara ya Mazingira ya Halmashauri, zimewasilisha mipango ya kujiandaa na kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.
Mikakati hiyo imewekwa kufuatia tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, TMA, kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa mvua kubwa katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Brigedia Jenerali Sakulo amewataka viongozi na watendaji kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hatua za kuchukua kabla na wakati wa mvua, ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuimarisha usafi wa mazingira, hususan katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na mafuriko, pamoja na kuchukua hatua za mapema katika kuimarisha miundombinu ya barabara na huduma ya umeme.
Aidha, Mhe. Sakulo amesisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema na ushirikiano kati ya taasisi za serikali, viongozi wa maeneo na wananchi, akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha Wilaya ya Ngorongoro inakuwa tayari kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.