Loliondo FM
Loliondo FM
7 November 2026, 9:42 pm

Na Saringe Saitoti
Jumla ya wanafunzi 14 kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wamepata ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kupitia mpango wa Ngorongoro Scholarship Fund, unaotekelezwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Wanafunzi hao wameagwa jijini Dar es Salaam kuelekea katika vyuo vikuu mbalimbali nchini baada ya kukidhi vigezo vya ufadhili huo, kati ya maombi 26 yaliyopokelewa na kufanyiwa uchambuzi.
Akizungumza katika hafla ya kuwaaga wanafunzi hao, Kamishna wa Uhifadhi wa Ngorongoro, Dkt. Abdul-Razaq Badru, amesema mpango huo uliozinduliwa Agosti 4, 2026, unalenga kuongeza fursa za elimu ya juu kwa wakazi waishio ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Dkt. Badru amesema kwa mwaka huu, NCAA imetenga shilingi milioni 100 kwa ajili ya mpango huo, huku akieleza kuwa wanafunzi watakaohitimu watanufaika na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa katika taasisi za Serikali na sekta binafsi.
Amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya NCAA katika maeneo matatu muhimu ambayo ni uhifadhi, utalii na kuboresha ustawi wa jamii zinazoishi ndani ya hifadhi.
Wanafunzi hao 14 wamepata udahili katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, Chuo cha Uhasibu Arusha (AIA) na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT).
Watahitimu katika fani zinazohusiana na uhifadhi wa wanyamapori, misitu, malikale na utalii, ambazo ni miongoni mwa maeneo muhimu katika uhifadhi na maendeleo ya sekta ya utalii nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Dkt. Bill Kiwia, amesema kati ya maombi 26 yaliyowasilishwa, wanafunzi 14 wamekidhi vigezo na kuchaguliwa kunufaika na ufadhili huo.
Ameeleza kuwa jumla ya shilingi milioni 70.6 zitatumika kugharamia masomo yao, akisisitiza kuwa mchakato wa uchaguzi umezingatia misingi ya haki, usawa na uwazi.
Naye Katibu wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro, James Moringe, ameipongeza Serikali kupitia NCAA kwa kuendelea kuwekeza katika elimu kwa wakazi wa Ngorongoro.
Amesema jitihada hizo zimewanufaisha wanafunzi katika ngazi mbalimbali za elimu, zikiwemo wanafunzi 93 wa sekondari, wanafunzi 33 wa kidato cha tano na sita, wanafunzi 36 wa vyuo vya kati na wanafunzi 14 wa vyuo vikuu waliochaguliwa mwaka huu.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Ndina Koyaki Mollel kutoka Kata ya Alailelai ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kupata fursa ya elimu ya juu, akisema ufadhili huo utawasaidia kutimiza ndoto zao, kujiajiri, kuajiriwa na kuchangia maendeleo ya familia na jamii zao.
Mpango wa Ngorongoro Scholarship Fund unatarajiwa kuendelea kutekelezwa kila mwaka kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, kwa kuzingatia mwongozo wa utoaji wa mikopo na ufadhili wa elimu ya juu.