Majengo ya WFP Isaka Kahama yakabidhiwa serikali
December 9, 2024, 9:19 am
Shirika la chakula duniani World Food Programme (WFP) limekabidhi kwa serikali majengo na ardhi iliyokuwa ikitumia katika Kata ya Isaka Wilayani Kahama mkoani Shinyanga yenye ukubwa wa hekari saba sawa na kilomita za mraba 29,450.
Na Paschal Malulu-Huheso FM KAHAMA
Hatua hiyo imefikiwa mara baada ya shirika hilo la WFP kusitisha shughuli zake katika eneo hilo tangu mwezi Januari mwaka huu 2024 ambapo imehamishia shughuli zake mkoani Dodoma.
Naibu mkurugenzi wa shirika la chakula duniani kwa upande wa Tanzania, Christine Mendes, akizungumza wakati wa kukabidhi amesema shughuli zao katika eneo hilo zinamalizika kuanzia Disemba 05, 2024 ambayo inatambulika WFP ISAKA LOGISTICS HUB HANDOVER.
Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa shirika la reli nchini TRC, John Mamuya ambaye ni meneja kanda ameiomba serikali ya Wilaya ya Kahama kuwapatia eneo hilo kwa ajili ya matumizi ya shirika kwani tangu awali walikuwa wakishirikiana na WFP tangu awali.
Nae diwani wa Kata ya Isaka, Pazi Majuto akizungumza kwa niaba ya wananchi wa eneo hilo amesema kuwa wameumia kuondoka kwa shirika hilo kwani lilikuwa nguzo kubwa ya Uchumi wa wananchi Pamoja na Kata yake huku akiiomba serikali kuwapatia majengo hayo.
Katibu tawala wa Wilaya ya Kahama, Hamad Mbega akimwakilisha mgeni rasmi mkuu wa Wilaya ya Kahama, amesema kuwa maombi yote wameyachukua na vikao rasmi vya kiserikali vitaamua hatima ya matumizi ya eneo hilo Pamoja na majengo yaliyopo.
Hata hivyo shirika la chakula duniani WFP lilianza shughuli zake katika eneo hilo miaka ya 1996 kwa lengo la usafirishaji wa chakula Kwenda katika kambi za wakimbizi zilizopo hapa nchini.