Huheso FM

Madiwani Ushetu waliomba jengo lao Manispaa ya Kahama

September 10, 2024, 4:35 pm

Madiwani wa halmashauri ya Ushetu wameiomba serikali ya Mkoa wa Shinyanga kufanya utaratibu wa kuwarejeshea jengo lililopo manispaa ya Kahama ambalo lilikuwa likimilikiwa na halmashauri hiyo kabla ya kujitenga na kuzalishwa kwa halmashauri ya Ushetu na Msalala.

Wakiongea kwenye kikao cha mwaka cha Baraza la Madiwani, madiwani hao wamesema kuwa wanaomba kurejeshewa jengo hilo ili liwasaidia kama chanzo cha mapato katika halmashauri yao.

Sauti za madiwani wakizungumza kwenye kikao cha madiwani

Katika hatua nyingine madiwani hao wamesema kuwa kila wanapofunga hesabu za mwaka za mali za halmashauri jengo hilo linahesabiwa lakini haliingizi mapato hali inayosababisha kuendelea kupata hati chafu katika halmashauri yao huku mwenyekiti wa halmshauri hiyo Gagi Lala akisema kuwa majengo hayo ni mali ya halmashauri ya Ushetu na Msalala baada ya kugawana.

Sauti ya diwani akizungumzia ukosefu wa mapato kupitia jengo hilo

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya ufuatiliaji wa menejimenti na ukaguzi mkoa wa Shinyanga Ibrahim Makana akiongea kwa niaba ya katibu tawala mkoa wa Shinyanga amesema kuwa mali zote za serikali zinakuwa kwenye mfumo maalum na kwamba serikali inaendelea kufuatilia suala hili kwa ukaribu na jambo hilo lipo ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali kwa ajili ya maamuzi yake.

Sauti ya katibu tawala msaidizi akizungumzia sehemu ya ufuatiliaji wa jengo hilo

Halmashauri ya Ushetu imeanzishwa rasmi mwaka 2013 ambapo kabla ya hapo ilikuwa halmashauri ya wilaya ya Kahama ikijumuisha eneo la Kahama Mjini, Ushetu na Msalala.