Huheso FM

Kahama: Soko la Phantom halina maji, vyoo

August 20, 2024, 2:37 pm

Picha ya soko la Phantom linalokabiliwa na changamoto ya huduma ya vyoo.

Na Rose Dominick, Lilian Francis

Wafanyabiashara wa soko la Phantom lililopo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wamelalamikia uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Nyasubi kwa kushindwa kukamilisha huduma ya choo hali inayosababisha watumiaji wa soko hilo kuvuka ng’ambo ya barabara kupata huduma.

Wafanyabiashara hao wakizungumza Agosti 20, 2024 na Huheso FM wamesema kuna changamoto ya huduma ya choo ambapo wanalazimika kuvuka ng’ambo ya barabara kupata huduma hiyo kutokana na soko hilo kukosa miundombinu ya vyoo.

Sauti za wafanyabiashara wakizungumzia kero ya ukosefu wa vyoo

Kwa upande wake mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Nyasubi Bw. Innocent Kapere amesema changamoto ya ukosefu wa vyoo katika soko hilo unatokana na kuchelewa kufungwa kwa mita na mabomba ya maji, pamoja na msimamizi wa vyoo ambaye atahusika na ukusanyaji wa mapato yanayotokana na vyoo hivyo.

Pia amewaomba wafanyabiashara kuendelea kuwa na subira pamoja na uvumilivu kwani changamoto hiyo inaenda kukamilika ndani ya mwezi huu wa Agosti.

Sauti ya mwenyekiti akijibu malalamiko kuhusu changamoto ya vyoo.

Aidha wafanyabiashara wa soko hilo wameupongeza uongozi kwa kuhakikisha ulinzi na usalama umeimarika katika soko lao kwani wanafanya kazi kwa amani na hakuna kesi za wizi katika eneo hilo.