Gari la uzoaji taka lazua malalamiko Kahama
August 19, 2024, 2:51 pm
Na, Neema Yohana, Veronica Kazimoto
Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Nyasubi Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga wameiomba serikali ya mtaa wa Nyasubi Kutatua changamoto ya kuchelewa kwa gari linalotumika kukusanya taka zinazozalishwa kwenye makazi yao.
Wametoa ombi hilo wakati wakizungumza na Huheso Fm Radio kwa Nyakati tofauti hii leo August 19 mwaka huu wamesema gari la uzoaji taka limekua na muda bila kupita kwenye maeneo yao kutokana na sababu inayotajwa kuwa ni matengenezo ya miundombinu ya barabara.
Wamesema wanaiomba serikali kuwatafutia njia mbadala itakayowasaidia kutoa taka hizo katika maeneo yao ya makazi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Nyasubi, Leonard Mayala amewataka wananchi kutoa taarifa mapema wanapokuwa na tatizo la kutofikiwa na gari hilo kwa ajili ya kupata usaidizi.
Aidha Mtaa wa Nyasubi ni miongoni mwa mitaa inayohudumiwa na zabuni ya uzoaji taka ambazo huzalishwa kutoka kwenye makazi hivyo gari la uzoaji taka katika mtaa wa Nyasubi hupita mara moja kwa wiki siku ya ijumaa.