Huheso FM

Mkoa wa Shinyanga watajwa kuongoza kwa ukatili

May 15, 2024, 11:17 am

Mwenyekiti wa umoja wa wanawake mkoa wa Shinyanga UWT Grace Bizulu

Vitendo vya ukatili kwa watoto hasa ulawiti wa watoto wa kiume zimeendelea kushamiri huku akina mama wakitajwa kutochukua hatua ya kuwalinda watoto.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga, Grace Bizulu amewataka wazazi na walezi mkoani humo kutowaacha nyuma kundi la watoto wa kiume katika kuwaepusha na ukatili wa kijinsia.

Bi. Bizulu amesema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano uliowahusisha UWT pamoja na wananchi katika kata ya Kitangili ambapo amesema wimbi kubwa la matukio la ukatili wa kijinsia linawaandama watoto wa kiume kwa sasa.

Amesema ukatili wa kijinsia umeongezeka kwa mkoa wa Shinyanga hivyo akina mama wanalo jukumu la kuhakikisha wanakaa karibu na watoto.

Sauti ya mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Shinyanga, Grace Bizulu wakati akizungumza kuhusu ukatili wa kijinsia

Aidha amewataka wanawake wote mkoa wa Shinyanga kuhakikisha wanamtanguliza Mungu kwa kufanya maombi ili Mungu aiepushe jamii na mmomonyoko wa maadili kwani maovu yote wanatupiwa lawama wanawake hivyo wawe msitari wa mbele.