Hakuna kupita bila kupingwa-ACT Wazalendo
May 11, 2024, 5:00 pm
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni mwenyekiti wa ACT – Wazalendo Taifa, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amekabidhiwa uchifu (utemi wa nchi) na wazee wa Kahama, kuwa mtemi/chifu wa kabila la wasukuma na wanyamwezi.
Zoezi hilo limefanyika wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, wakati wa ziara ya kiongozi huyo mkuu wa ACT – Wazalendo, akiwa katika mkutano wa hadhara katika kata ya Kagongwa manispaa ya Kahama.
Akiwahutubia wananchi hao, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amewataka watanzania kukubali mageuzi ili kuwaletea wananchi maendeleo kulingana na rasilimali walizonazo.
“Kwa hiyo ndugu zangu ninachowakumbusha, kwamba ni lazima kama nchi hii mnataka rasilimali ilizonazo zitafsiriwe kuwa utajiri kwa kila mtu, mnataka rasilimali tulizonazo ziwe na maslahi kwa watanzania wote, hili liwe ni Taifa la wote, ni lazima tufanye mageuzi” Alisema Mheshimiwa Othman Masoud
“Ndugu zangu wanakahama, ujumbe wangu niliokuja nao ni kuwakumbusha kama tunaitaka Kahama itafsiri rasilimali zake kuwa Maisha ya watu, itafsiri rasilimali zake kuwa maendeleo ya kweli, mtukabidhi Kahama ACT – Wazalendo, kwa sababu tumewathibitishia tuna maono na sisi tuna ahadi yetu kwa Watanzania, viongozi wetu watapita kuieleza na kuifafanua” Aliongeza Mheshimiwa Othman
Awali akimkaribisha mwenyekiti kuzungumza na wananchi, kiongozi mstaafu wa ACT – Wazalendo Zitto Kabwe, aliwataka wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu, ili kujiandaa vyema na uchaguzi mkuu wa mwakani 2025.
Zitto aliwatoa hofu wanachama wa chama hicho kuondoa hofu ya kutokutangazwa baada ya uchaguzi, kwani tayari chama hicho kinaendelea na jitihada za maboresho ya sharia za uchaguzi pamoja na kusimamia katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kila Mtanzania awezekupata haki yake ya kikatiba.