Kishimba aomba tiba bure kwa wananchi kama ilivyo kwenye elimu
March 15, 2024, 11:47 am
”Tunaendelea kuiomba serikali katika swala la matibabu ilitazame kwa jicho la upana sana kuwasamehe watoto shule na matibabu pia iwe bure kwa sababu ni kitu cha lazima” amesema Mbunge Kishimba.
Na Neema Nkumbi- Huheso Fm
Kituo cha afya Kagongwa kinachohudumia wananchi takribani 60,000 wa Kata za Kagongwa, Mondo na Isagehe kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kimepokea gari la kubebea wagonjwa [Ambulance] kwa ajili ya wagonjwa kupata huduma.
Gari hilo limekabidhiwa March 14, 2024 na Mbunge wa Jimbo la Kahama mji Jumanne Kishimba katika hafla ya makabidhiano yaliyofanyika Kata ya Kagongwa Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga, Kishimba amesema kuwa gari hilo limekabidhiwa ili kuokoa uhai wa wananchi hivyo hawana budi kulitunza.
Wananchi wa Kata ya Kagongwa wamesema kuwa kupatikana kwa gari hilo kutasaidia kuokoa uhai wa wagonjwa hasa wanawake na watoto wanao kabiliwa na changamoto nyingi za kiafya.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama Dr Fredrick Malunde licha ya kupokea gari hilo anatambua uwepo wa changamoto ya upungufu wa watumishi kwenye kituo hicho atahakikisha wanaongezeka pindi serikali itakapotoa ajira.
Mara baada ya kukabidhi gari hilo mbunge Jumanne Kishimba amesema changamoto ya matibabu bado ni kubwa ataendelea kumwomba Mheshimiwa Rais Samia kupitia bunge kufanya matibabu kuwa bure kama ilivyo elimu bure kwa sasa.