Wananchi wachangia milioni 16 ujenzi wa vyumba vya madarasa Kahama
March 8, 2024, 10:38 am
Serikali ya mtaa wa Mhongolo Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga imeelezea namna ilivyotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kushirikiana na wananchi wa mtaa huo.
Imesema kuwa zaidi ya shilingi milioni 16 nguvu za wananchi zilitumika katika ujenzi wa boma la vyumba sita vya madarasa na ofisi moja ya walimu pamoja na matundu tisa ya vyoo katika shule mbili za Mhongolo katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Neema Nkumbi-Huheso FM
Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake Mwenyekiti wa Mtaa huo, Emmanuel Nangale amesema wananchi wanashiriki bega kwa bega katika shughuli za Ujenzi wa Miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo matundu tisa ya vyoo yamejengwa katika shule ya Sekondari Nyashimbi, na vyumba vinne vya madarasa na ofisi ya walimu vimejengwa katika shule ya msingi Bomani.
Hata hivyo mwenyekiti huyo amesema kuwa licha ya miradi hiyo Wananchi wameweza kushiriki kikamilifu katika upandaji wa miti 2000 katika shule ya msingi Bomani.
Pia Nangale amebainisha kuwa Kata ya Mhongolo ni mojawapo kati ya Kata kubwa katika Manispaa ya Kahama na kuongeza kuwa kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 inaonesha kuwa Kata ya Mhongolo ina wakazi takribani 44,000 huku mtaa wa Mhongolo pekee ukiwa na wakazi 21,000.
Aidha akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Mtaa wa Mhongolo, Abdalah Suleiman amesema kuwa kama wananchi wanapokea miradi hiyo kwa mikono miwili kwa sababu inawagusa moja kwa moja mfano Zahanati, Shule, Maji pamoja na Umeme.
Amesema kama wananchi wamekuwa wakishiriki kikamilifu kwa kuchangia kiasi ambacho wanapaswa kuunga juhudi mkono serikali ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inaendelea pasipo kusimama na baadaye inawasaidia wao.