TBS yatoa mafunzo ya vifungashio kwa wajasirimali wa mchele Kahama
April 28, 2021, 2:18 pm
Wajasiliamali 100 ambao ni wasindikaji, wauzaji na wasambazaji wa Mchele Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wamepatiwa mafunzo kuhusu kanuni bora za uzalishaji na taarifa za msingi zinazotakiwa kuwepo kwenye vifungashio na shirika la viwango nchini TBS.
Mafunzo hayo yametolewa kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama huku mgeni rasmi akiwa mkuu wa Wilaya ya Kahama Anamringi Macha ambaye amesema kwa sasa zao hilo limekuwa la kibiashara kutokana kuwa na soko hadi nje ya nchi.
Akifungua Mafuzo hayo amesema wajasiliamali nchini ikiwa ni pamoja na wazalishaji, wauzaji na wasambazaji wa mchele wanatambulika kuwa sehemu ya washiriki wa kukuza uchumi wa Taifa kwani wanamchango mkubwa katika kukuza pato la taifa na kutengeneza ajira kwa wananchi.
Kwa upande wake meneja utafti na mafunzo wa shirika la viwango Tanzania TBS, Hamis Sudi Mwanasala amesema mafunzo hayo yamekuwa maalum kwa sababu yamechangizwa na maadhimio yaliyotokana na kikao cha wadau wa Mchele kuomba kupewa elimu ya ubora wa vifungashio na uwekezaji wa Mchele ili wapate masoko.
Hata hivyo Mafunzo hayo yatafanyika sehemu tatu za kanda ya ziwa ikiwemo Kahama mkoani Shinyanga, Bukombe mkoani Geita na Sengerema mkoani Mwanza lengo ni kutoa elimu kwa wawekezaji wa sekta ya Mchele juu ya matakwa ya viwango, uhifadhi, ubora na vifungashio.