Radio Jamii Kilosa

TFS Kilosa yasisitiza sheria za uvunaji mazao misitu

13 April 2026, 5:11 pm

Mhifadhi Deus Bijanju akiwa katika kipindi maalumu katika studio za Redio Jamii Kilosa. Picha na Beatrice Majaliwa

Uvunaji wa mazao ya misitu una umuhimu mkubwa kiuchumi, kimazingira na kijamii, hususan unapofanyika kwa kufuata taratibu za Tanzania Forest Services Agency (TFS), ni nyenzo muhimu ya maendeleo, lakini usipodhibitiwa unaweza kuleta madhara makubwa kwa mazingira na jamii.

Na Asha Madohola

Mhifadhi wa misitu kutoka Tanzania Forest Services Agency (TFS) wilayani Kilosa, Deus Daniel Bijanju amesema kuwa TFS ina jukumu la kusimamia, kulinda na kuhakikisha matumizi endelevu ya misitu pamoja na kusimamia shughuli za ufugaji nyuki kwa manufaa ya taifa.

Aidha, mhifadhi huyo ameeleza kuwa TFS pia inasimamia utaratibu wa uvunaji wa mazao ya misitu kwa kuhakikisha unafanyika kwa kufuata sheria, kanuni na vibali rasmi vinavyotolewa na mamlaka husika.

Amesisitiza kuwa uvunaji holela wa mazao ya misitu unasababisha uharibifu wa mazingira, hivyo ni muhimu wananchi kufuata taratibu zilizowekwa ili kulinda rasilimali hizo muhimu.

Mhifadhi wa TFS Kilosa Deus Bijanju

Akizungumzia changamoto, amesema TFS inakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya wananchi kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu utunzaji wa mazingira, hali inayochangia uvunaji usiofuata sheria na uharibifu wa misitu.

Hata hivyo, ameongeza kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia mikutano, semina na ushirikiano na viongozi wa vijiji ili kuongeza uelewa.