Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
19/03/2026, 14:19

Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS) ni mfumo wa kidijitali unaotumiwa na TRA kurahisisha huduma za kodi kwa walipakodi unaorahisisha wafanyabiashara kufanya malipo ya kodi.
Na Aloycia Mhina
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Kilosa imewataka wafanyabiashara wilayani hapa kujitokeza mapema katika ofisi za mamlaka hiyo kwa ajili ya kukadiriwa kodi, huku ikieleza kuwa mwezi Machi ni kipindi rasmi cha zoezi la makadirio ya kodi linaloendelea hadi Desemba 31 mwaka huu.
Akizungumza na Redio Jamii Kilosa, Meneja wa TRA Wilaya ya Kilosa, Bwana Laston Thoby Mkarlu, amesema kuwa ni muhimu kwa wafanyabiashara kutumia fursa ya mwezi huu wa makadirio kwa kufika mapema na kuwasilisha taarifa sahihi za mapato yao ili kukamilisha taratibu kwa wakati.
Ameeleza kuwa wafanyabiashara wanapaswa kuandaa nyaraka na hesabu zao kwa umakini, kwani kuchelewa kufanya makadirio kunaweza kusababisha adhabu au riba zisizo za lazima. Ameongeza kuwa kufanya makadirio kwa wakati ni njia bora ya kuepuka usumbufu na kuhakikisha uzingatiaji wa sheria za kodi.
Aidha, Bwana Mkarlu amebainisha kuwa walipakodi wanaokadiriwa ni pamoja na wale wenye mapato yasiyozidi shilingi milioni 100 kwa mwaka, huku akiwahimiza wafanyabiashara wakubwa na wenye makampuni kutumia Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS), unaorahisisha huduma mbalimbali ikiwemo ulipaji kodi, marekebisho ya risiti, na maombi ya msamaha wa riba au kodi, hivyo kupunguza kero kwa walipakodi.