Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
12/03/2026, 14:08

Vodacom Tanzania Foundation imewadhamini madaktari bingwa kutoa huduma za matibabu kupitia kambi ya afya bure kwa wananchi ambapo inalenga kupima na kutibu magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, matatizo ya macho, meno na tezi dume.
Na Asha Madohola
Madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili wamewasili Wilayani Kilosa kutoa huduma za matibabu kupitia kambi maalum ya upimaji na matibabu ya afya bure kwa wananchi wa wilayani hapa na maeneo ya jirani.
Kambi hiyo inalenga kuwapatia wananchi fursa ya kupata uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali bila gharama, hususan magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiongezeka katika jamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo muhimu ili kufahamu hali ya afya zao na kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake za kuendelea kuimarisha sekta ya afya nchini, akieleza kuwa kwa sasa huduma za afya zimeboreshwa kwa kiasi kikubwa huku dawa na vifaa tiba vikipatikana katika vituo mbalimbali vya afya. Pia aliwapongeza Vodacom Foundation Tanzania kwa kudhamini kambi hiyo na kufanikisha ujio wa madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kutoa huduma kwa wananchi wa Kilosa na maeneo jirani.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na Daktari wa Magonjwa ya Dharura, Patrick Shayo, amesema madaktari hao wanatarajia kuwahudumia zaidi ya wananchi elfu mbili katika kipindi cha kambi hiyo na wapo tayari kutoa huduma kwa wananchi na huduma zitakazotolewa zote ni bureni.

Aidha, kambi hiyo imewezeshwa kwa ushirikiano wa taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation, ambapo Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation Bi Sandra Osward alisema wameendelea kushirikiana na wataalamu wa afya ili kuwasogezea wananchi huduma muhimu za matibabu na kupitia mpango huo wananchi wa Kilosa na maeneo ya jirani wanapata fursa ya kupimwa, kupata ushauri wa kitaalamu pamoja na kuanza matibabu bure.

Awali akizungumza Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wilayani Kilosa Selemani Kasugulu alisema shughuli zinazofanyika katika kambi hiyo ni pamoja matibabu ya magonjwa ya akinamama, meno, macho,tezi dume na wananchi zaidi ya mia tano kwa siku ya kwanza walijitokeza kupimaafya zao na matarajio kwa siku nne wananvhi wengi watakuwa wamepatiwa huduma za kiafya kutoka kwa madaktari bingwa.

