Radio Jamii Kilosa

Mhe Kombani atoa vifaa kwa watoto maalum Kilosa

12/03/2026, 11:03

Watoto wenye mahitaji maalumu ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi Ustawi na Ilonga Mazoezi wakiwa wamekabidhiwa zawadi kutoka kwa mbunge viti maalumu mkoa Morogoro Mhe Lucy Kombani. Picha na Farida Hassan

Kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu ni muhimu kwa sababu huwapa fursa sawa ya kupata elimu, huduma za afya na malezi bora kama watoto wengine na huchangia kupunguza unyanyapaa na kuhakikisha wanapata mazingira salama na bora ya kukua na kufikia ndoto zao.

Na Asha Madohola

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Mhe. Lucy Kombani, ametoa msaada wa madaftari ya kujifunzia pamoja na kalamu kwa watoto wenye mahitaji maalum wanaosoma katika Shule za Msingi Ustawi na Mazoezi zilizopo Kata ya Chanzuru, Kijiji cha Ilonga Wilayani Kilosa.

Msaada huo umetolewa kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi hao kupata vifaa muhimu vya kujifunzia na kuongeza hamasa yao ya kuhudhuria masomo kwa bidii.

Zawadi hizo zilikabidhiwa kwa niaba ya mbunge huyo na Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Morogoro, Bi. Joyce Hamis Nyangi, ambaye alisema kuwa Mhe. Lucy Kombani ameendelea kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha sekta ya elimu nchini.

“Mbunge huyo ametambua umuhimu wa kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum ili nao waweze kupata haki sawa ya elimu na kufikia ndoto zao za maisha na msaada huo ni ishara ya kujali na kuguswa kwa mbunge huyo na changamoto zinazowakabili watoto hao katika mazingira yao ya kujifunzia alisema Bi Nyangi”.

Sauti ya Mwenyekiti Smaujata mkoa wa Morogoro Bi Joyce Nyangi akizungumza
Mwenyekiti wa Smaujata mkoa wa Morogoro Bi Joyce Hamis Nyangi

Aidha, alibainisha kuwa Mhe. Lucy Kombani pia aliwapatia tuzo SMAUJATA Mkoa wa Morogoro kwa kutambua mchango wao mkubwa katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu kupinga ukatili wa kijinsia na kuhamasisha ulinzi wa haki za wanawake na watoto katika jamii.

Sauti ya Mwenyekiti Smaujata mkoa wa Morogoro Bi Joyce Nyangi akizungumza

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Chanzuru Philipo Mageni alimshukuru mbunge huyo kwa msaada huo akisema kuwa vifaa hivyo vya kujifunzia vitasaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa vifaa shuleni ambayo wakati mwingine husababisha baadhi ya wazazi wanashindwa kuhumudu mahitaji yao

Sauti ya Mhe diwani wa kata ya Chanzuru Philipo Mageni
Viongozi na wanafunzi wa shule ya msingi Ustawi katika picha ya pamoja

Kwa upande wake Mratibu Elimu kata ya Chanzuru Ndg Amon Lameck Ngolo alimshukuru Mhe Mbunge Viti Maalumu mkoa wa Morogoro kwa msaada wa madaftari kwa wanafunzi ambao watahudhuria masomo kikamilifu na kuongeza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza utoro shuleni, kuongeza ari ya wanafunzi kusoma pamoja na kuinua kiwango cha ufaulu katika shule hizo.

Sauti ya Mratibu Elimu Kata ya Chanzuru akizungumza

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hizo akizungumza kwa niaba ya walimu na wanafunzi, alimshukuru Mhe. Lucy Kombani kwa msaada huo akieleza kuwa umeleta faraja kubwa kwa watoto wenye mahitaji maalum. Hata hivyo aliomba wadau mbalimbali wa maendeleo na viongozi kuendelea kuwasaidia wanafunzi hao kwa misaada ya kielimu na kijamii ili kuboresha mazingira yao ya kujifunzia na kuhakikisha misaada kama hiyo haishii hapo bali inaendelea kuwafikia mara kwa mara.

Sauti ya Mwalimu Mkuu Theresia Mziray wa shule ya Msingi Ustawi akizungumza

Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, wanafunzi wanaosoma katika shule hizo akiwemo mwanafunzi Christian Emmanuel wametoa shukurani zao kwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Mhe. Lucy Kombani, kwa msaada wa madaftari na kalamu aliowapatia pia zawadi hiyo imewapa faraja na motisha ya kusoma kwa bidii zaidi ili kufikia malengo yao ya kielimu.

Sauti ya mwanafunzi Christian Emmanuel akizungumza