Radio Jamii Kilosa

DC Kilosa azindua chanjo ya mifugo

08/03/2026, 11:00

Mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe Shaka Hamdu Shaka akizindua zoezi la chanjo mifugo ili kudhibiti magonjwa. Picha na Beatrice Majaliwa

Chanjo ya mifugo ni dawa maalum inayochomwa wanyama kama ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku ili kuwakinga dhidi ya magonjwa mbalimbali na husaidia kupunguza vifo vya mifugo, kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama, pamoja na kuhakikisha mifugo inakuwa na afya bora.

Na Beatrice Majaliwa

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, alizindua rasmi zoezi la utoaji wa chanjo ya homa ya mapele ngozi kwa ng’ombe na homa ya mapafu kwa mbuzi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha afya ya mifugo na kuongeza uzalishaji kwa wafugaji wilayani hapa.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Shaka alisema chanjo hiyo itasaidia kudhibiti na kuzuia magonjwa mbalimbali ya mifugo yanayosababisha hasara kubwa kwa wafugaji, huku akibainisha kuwa Wilaya ya Kilosa ina idadi kubwa ya mifugo hivyo kuna uhitaji mkubwa wa chanjo kwa ajili ya kulinda afya ya wanyama hao.

Aidha, aliitaka kampuni ya Huthem inayoratibu zoezi hilo kuongeza juhudi katika uhamasishaji ili kuwafikia wafugaji wengi zaidi pamoja na kushirikiana na viongozi wa chama cha wafugaji ili kuhakikisha elimu kuhusu chanjo inawafikia wafugaji kwa urahisi.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe Shaka akizungumza
Mkurugenzi wa Kampuni ya Huthem, Bw. Humphrey Peter Maseu

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Huthem, Bw. Humphrey Peter Maseu, ameishukuru serikali kwa kuwezesha ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali katika kutekeleza zoezi hilo, ambapo utoaji chanjo limeratibiwa na Kampuni ya Huthem kwa kushirikiana na serikali.

Sauti ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Huthem, Bw. Humphrey Peter Maseu akizungumza
Mratibu wa chanjo kutoka kampuni ya Huthem, Bw. Maungo Omar Hamis

Mratibu wa chanjo kutoka kampuni hiyo, Bw. Maungo Omar Hamis, alisema kuwa wanatarajia kufikia mifugo zaidi ya laki moja na sabini wilayani Kilosa licha ya kuwepo kwa changamoto chache katika utekelezaji wa zoezi hilo.

Sauti ya Mratibu wa chanjo kutoka kampuni ya Huthem, Bw. Maungo Omar Hamis akizungumza

Naye Mkuu wa Idara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo Wilaya ya Kilosa, Bw. Elia Shemtoi, aliwataka wafugaji kutoa ushirikiano kwa kampuni hiyo ili kufanikisha zoezi la chanjo, endapo kutajitokeza watu ambao hawatambuliki kiwilaya watoe taarifa mapema ngazi husika.

Sauti ya Mkuu wa Idara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo Wilaya ya Kilosa, Bw. Elia Shemtoi akizungumza

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wilayani hapa, Bw. Mkunwa Suliani, alisema kuwa wafugaji wamepokea kwa furaha hatua hiyo kwani itasaidia kulinda mifugo dhidi ya magonjwa na kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama.

Sauti ya Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Kilosa, Bw. Mkunwa Suliani,akizungumza

Baadhi ya wafugaji waliohudhuria uzinduzi huo walisema kuwa zoezi la chanjo litasaidia kupunguza vifo vya mifugo pamoja na kuongeza tija katika ufugaji wao.