Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
05/03/2026, 10:24

Kisukari ni ugonjwa unaotokea pale mwili unaposhindwa kuzalisha au kutumia vizuri homoni ya insulini, hali inayosababisha kuongezeka kwa kiwango cha sukari kwenye damu na kupima mapema huokoa maisha na husaidia kuepuka madhara makubwa kama matatizo ya figo na magonjwa ya moyo.
Na Asha Madohola
Wananchi wilayani Kilosa wamehimizwa kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kubaini mapema magonjwa yasiyoambukiza, hususan kisukari ambacho kinaongezeka kwa kasi.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Magonjwa Yasiyopewa Kipaumbele kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, Daktari Alphonce Martin, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Radio Jamii.
Daktari Martin alisema uchunguzi wa mapema ni njia muhimu ya kujikinga na madhara makubwa ya kisukari, akibainisha kuwa wananchi wengi huchelewa kupima hadi wanapopata maumivu makali au dalili zinazoashiria hali kuwa mbaya, jambo linalochelewesha matibabu.

Alieleza kuwa kisukari hutokana na mwili kushindwa kutumia au kuzalisha insulini kwa kiwango kinachotakiwa, hali inayoongeza sukari kwenye damu na dalili zake ni pamoja na kukojoa mara kwa mara, kiu isiyoisha, kupungua uzito bila sababu, uchovu na vidonda visivyopona haraka, huku akisisitiza kuwa wakati mwingine ugonjwa huo hukaa mwilini bila dalili za wazi.
Kutokana na changamoto ya wagonjwa wengi kufika hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho, hali inayoweza kusababisha madhara kama ulemavu, matatizo ya figo na upofu, wananchi wamehimizwa kujitokeza kila Alhamisi hospitalini kwa uchunguzi, ushauri na matibabu bila kusubiri hali kuwa mbaya.