Radio Jamii Kilosa

Vitamin A, dawa za minyoo zatolewa Kilosa

16 December 2025, 11:03 am

Maafisa Lishe wilayani Kilosa wakiwa kwenye kipindi maalumu cha mwezi wa afya na lishe kwa mtoto. Picha na Stamius Kyombo

Mwezi wa Afya na Lishe ni kampeni ya kitaifa inayofanyika kila mwaka kuanzia Desemba 1 hadi 31, yenye lengo la kuboresha afya ya mama na mtoto kwa kutoa huduma muhimu za lishe katika vituo vya kutolea huduma za afyana huduma hizo hutolewa bila malipo na hulenga zaidi watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Na Asha Madohola

Katika kipindi hiki, watoto wenye umri wa kuanzia miezi 6 hadi miaka 5 hupatiwa Vitamin A, ambayo ni muhimu kwa kuongeza kinga ya mwili, kuzuia upofu unaosababishwa na ukosefu wa vitamini hiyo, pamoja na kupunguza hatari ya vifo vya watoto wadogo. 

Wito huo ulitolewa Maafisa Lishe wilayani Kilosa Elisha Kingu na Martha Damiano katika kipindi cha Ijue Halmashauri Yako kinachorushwa na Redio Jamii Kilosa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya mwezi wa afya na lishe.

Afisa Lishe Kingu akitoa ufafanuzi kuhusu umuhimu wa kampeni ya mwezi wa faya na lishe kwa mtoto

Aidha, watoto hupatiwa dawa za minyoo ambazo husaidia kupunguza maambukizi ya minyoo tumboni, hali inayosababisha udumavu, utapiamlo, na kushuka kwa uwezo wa mtoto kujifunza.

Wazazi na walezi walihimizwa kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya afya vilivyo karibu ili kuhakikisha watoto wanapata huduma hizi kwa wakati, kwa ajili ya ukuaji bora, afya njema, na maendeleo ya watoto katika jamii.