Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
1 December 2025, 11:32 am

Chakula shuleni husaidia kupunguza utoro na kuimarisha mahudhurio kwa kuwa watoto wengi huhamasika kwenda shule wakijua watapata chakula na, huwasaidia watoto wa familia zisizo na uwezo mkubwa kupata mlo kamili angalau mara moja kwa siku, hivyo kupunguza athari za utapiamlo na maradhi ya upungufu wa virutubishi.
Na Asha Madohola
Kitengo cha lishe katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa leo kimefanya kikao maalum cha maandalizi ya bajeti ya afua za lishe kwa mwaka wa fedha 2026/2027, kikihusisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya afya, elimu, mifugo na kilimo.
Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Lishe wa Wilaya, Elisha Kingu, amesema kuwa bajeti ya mwaka huu inakadiriwa kufikia shilingi milioni 137, ambapo imejikita kushughulikia changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa afua za lishe mwaka uliopita.

Elisha Kingu ameorodhesha changamoto kadhaa zikiwemo uwepo wa takwimu zisizo sahihi kutoka ngazi ya jamii na vituo vya afya, idadi ya wanafunzi wanaopata chakula shuleni bado ni ndogo huku uelewa wa wahudumu wa afya wa jamii kuhusu lishe ukiwa ni mdogo.
Kwa upande wake, Afisa Mifugo Faraja Sanga ametoa wito kwa wananchi kufuga mifugo ili kusaidia upatikanaji wa vyakula vyenye asili ya wanyama kama vile maziwa na mayai ambavyo ni muhimu kwa lishe bora, hasa kwa watoto na akina mama wajawazito hukuakisisitiza kuwa ufugaji wa kisasa unaweza kusaidia kupunguza tatizo la lishe duni kwa kuongeza upatikanaji wa protini katika jamii.

Naye Nelson Kiliba, Afisa Elimu anayeshughulikia vifaa na takwimu, ambaye alimwakilisha Afisa Elimu Msingi, amesema hali ya lishe mashuleni ni mbaya kutokana na wanafunzi wengi kutopata chakula wakiwa shuleni, hali inayochangia kushuka kwa taaluma pia ametoa wito kwa wazazi na walezi kuchangia kwa hiari huduma ya chakula ili watoto waweze kujifunza wakiwa na afya bora na umakini darasani.
