Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
27 November 2025, 5:54 pm

Changamoto kubwa zinazokumba lishe kwa watoto na akina mama ni pamoja na ukosefu wa uelewa kuhusu lishe sahihi, umasikini, upatikanaji mdogo wa vyakula vya lishe, na mila au desturi zisizozingatia mahitaji ya lishe. Hali hii husababisha utapiamlo, upungufu wa damu, na kudumaa kwa watoto.
Na Asha Madohola
Katika kuadhimisha Siku ya Lishe Kitaifa mwaka 2025, maafisa lishe wilayani Kilosa wamefanya zoezi maalum la uhamasishaji na utoaji wa elimu ya lishe kwa jamii, kwa kutembelea vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya kuanzia tarehe 17 hadi 21 Novemba.
Katika ziara hizo, maafisa lishe Elisha Kingu, Martha Damiano, Rose Kavushe, Salha Juma, Jackson Kalibwani, Keraryo Maginga na Zaina Kibona wametembelea vituo vya afya vya Ruaha, Misheni, Kidodi, Ulaya, Zombo, Magomeni, Kimamba, Rudewa, Dumila, Msowero na Magubike. Wametumia nafasi hiyo kutoa elimu kuhusu umuhimu wa matone ya vitamin A kwa watoto kwa ajili ya kinga dhidi ya maradhi na kuimarisha ukuaji wao.
Akizungumza Afia lishe wilaya ya Kilosa Elisha Kingu alisema lengo kuu ni kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa mama na mtoto, pamoja na maandalizi ya kampeni ya kitaifa ya ugawaji wa vitamin A inayotarajiwa kuanza rasmi Desemba 1, 2025.

Afisa Lishe Zaina Kibona ametumia fursa ya kipindi maalum redioni kupitia Radio Jamii Kilosa kutoa elimu ya kina kwa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa watoto na akina mama. Ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanazingatia utoaji wa vyakula vyenye virutubisho muhimu ili kujenga afya na kuimarisha kinga za miili ya watoto, sambamba na kuhimiza unyonyeshaji wa maziwa ya mama katika miezi sita ya mwanzo bila kuwapa vyakula vingine.

Kwa upande wake, Afisa Lishe Salha Juma amewahamasisha akinamama wajawazito na wanaonyonyesha kuhakikisha wanapata lishe bora kwa ajili ya afya zao na ukuaji salama wa watoto wao huku Afisa Lishe Rose Kavishe akiwaeleza wazazi umuhimu wa kunyonyesha watoto ipasavyo na jinsi ya kuandaa chakula chenye lishe bora nyumbani pia alitoa maelekezo ya namna ya kuchanganya makundi sita ya vyakula ili kupata mlo kamili kwa watoto na familia kwa ujumla.

Naye Martha Damiano, ambaye pia ni Afisa Lishe, ameelezea mafanikio ya utoaji elimu hiyo kwa jamii ambapo wameweza kuwafikia watu wengi, huku akisisitiza kuwa lishe bora ni msingi wa ukuaji mzuri wa mtoto, kuimarisha uwezo wa kujifunza na kuepuka magonjwa yanayotokana na lishe duni.
