Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
18 November 2025, 6:17 pm

Hapa nchini katika baadhi ya shule bado kuna changamoto kubwa ya idadi ndogo ya wanafunzi wanaopata huduma ya chakula cha mchana mashuleni na inaelezwa tatizo hili linachangiwa na wazazi wengi kutokuwa na utayari wa kuchangia chakula hasa kwa watoto wasio katika madarasa ya mitihani ambapo hali hiyo inathiri moja kwa moja maendeleo ya kitaaluma ya wanafunzi, hali ya lishe na afya zao kwa ujumla.
Na Asha Madohola
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Bi. Beatrice Clavery Mwinuka, ametoa wito mzito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanachangia chakula mashuleni ili kuimarisha afya na ufaulu wa wanafunzi.
Alitoa wito huo Novemba 17, 2025 wakati wa kikao cha kujadili utekelezaji wa afua za lishe kwa robo ya kwanza (Julai–Septemba) kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri, kikihusisha wadau mbalimbali kutoka idara ya fedha, mipango, kilimo, uvuvi, mifugo, elimu msingi na sekondari, pamoja na mwanasheria wa halmashauri.
Bi. Mwinuka amesema kuwa suala la watoto kupata mlo wa mchana shuleni si jambo la hiyari tena, bali ni hitaji muhimu linalopaswa kuzingatiwa kwa mustakabali wa elimu bora kwa watoto huku akiagiza kamati za lishe mashuleni na vijijini kuendelea kuhamasisha uchangiaji wa chakula na kuhakikisha chakula hicho kinakuwa na viambata muhimu vya lishe.
Katika kikao hicho, Bi. Mwinuka amewataka wadau wa lishe kutoka kila idara kuhakikisha wanatoa taarifa za utekelezaji wa mpango wa lishe kila baada ya robo mwaka, sambamba na kuwa makini katika utoaji wa tenda kwa wazabuni wa chakula, ili kuhakikisha vyakula vinavyosambazwa mashuleni vinakuwa na ubora na vimeongezewa virutubishi.

Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Bi. Martha Damiano, ameeleza kuwa bado kuna idadi ndogo ya wanafunzi wanaokula chakula mashuleni na uhaba wa viwanda vya kuongeza virutubishi kwenye vyakula na amependekeza hatua mbalimbali zikiwemo kuhamasisha kilimo cha shule, na kuhakikisha unga unaonunuliwa na shule kutoka kwa wazabuni umeongezewa virutubishi.

Mwanasheria wa Halmashauri Tausi Heri Mbonile amesema kuwa ofisi yake iko katika hatua za mwisho kuandaa sheria ndogo ndogo zitakazolenga kuwabana wazazi na walezi kushiriki kikamilifu kwenye uchangiaji wa chakula na kwamba sheria hizo zitapelekwa katika vijiji kwa ajili ya kujadiliwa na kuanza kutumika, ambapo lengo kuu ni kuhakikisha kila mzazi anawajibika kuhakikisha mtoto wake anapata lishe bora akiwa shuleni.
