Radio Jamii Kilosa

Jamii yahimizwa kujitokeza kupima saratani ya matiti mapema

6 October 2025, 2:30 pm

Afisa Muuguzi kutoka hospitali ya wilaya ya Kilosa Bi Joyna Mlwale akitoa mafunzo kwa watendaji kata katika ukumbi Maktaba uliopo hospitali hapo. Picha na Elizabeth Makemba

Saratani ya matiti inaweza kutibika iwapo itagundulika mapema. Njia za kuzuia ni pamoja na kujichunguza mara kwa mara, kupima kliniki, kuishi maisha yenye afya, na kuepuka vihatarishi kama vile unywaji wa pombe kupita kiasi na uvutaji wa sigara.

Na Asha Madohola

Jamii Wilayani Kilosa na Mkoa wa Morogoro kwa ujumla imehimizwa kujitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti, ili kuweza kubaini ugonjwa huo mapema na kuanza matibabu kwa wakati.

Wito huo ulitolewa wakati wa mafunzo maalum kwa viongozi wa kata, viongozi wa dini na waathirika wa saratani ya matiti yaliyofanyika katika ukumbi wa maktaba wa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Dkt. Salvatory Kyara, Daktari wa Upasuaji kutoka Hospitali ya Rufaa ya Morogoro, alisema saratani ya matiti ni ugonjwa hatari unaosababisha vifo vingi, lakini unaweza kuzuilika endapo utagundulika mapema na kwamba saratani hiyo husababishwa na mabadiliko ya vinasaba, mtindo wa maisha usiofaa, lishe duni, matumizi ya pombe na kutofanya uchunguzi mara kwa mara.

Sauti ya Dkt Salvatory Kyara akizungumza

Naye Afisa Muuguzi Joyna Vitus Mlwale, ambaye pia ni Kaimu Mratibu wa Huduma za Mama na Mtoto, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watendaji wa kata juu ya namna ya kutambua dalili za awali za saratani ya matiti, visababishi vyake, na namna sahihi ya kujipima ili kuongeza uelewa kwa jamii nzima kupitia viongozi wao.

Sauti ya Afisa muuguzi Bi Joyna Mlwale akizungumza

Kwa upande wake, Saimon Bartazar Swai, Katibu wa Afya Wilaya (akimwakilisha Mganga Mkuu wa Wilaya), aliishukuru taasisi ya Jhpiego kwa kufanikisha mafunzo hayo muhimu, huku akisisitiza kuwa elimu hiyo ifikishwe kwa jamii kupitia watendaji waliopata mafunzo.

Sauti Katibu wa Afya Saimoni Swai akizungumza

Viongozi wa kata zaidi ya 40, viongozi wa dini na baadhi ya waathirika walihudhuria mafunzo hayo, ambapo akizungumza kwa niaba ya viongozi wakata Mtendaji wa kata ya Dumila Hamza Ally ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti katika mafunzo hayo alisema wanashukuru kwa elimu waliyopewa yatakayowasaidia kuwahamasisha wananchi kuhusu saratani ya matiti huku wakiomba elimu hiyo iwe endelevu.

Sauti ya Mtendaji Kata ya Dumila akizungumza