Radio Jamii Kilosa

Wakazi wa Kilosa watakiwa kuzingatia ufugaji bora wa mbwa

24 September 2025, 6:22 pm

Pichani ni mbwa mbao hawajafugwa vizuri na kusababisha hatari kwa binadamu. Picha na mtandaoni

Maadhimisho ya wiki ya kichaa cha mbwa yanatarajiwa kufanyika 28 Septemba 2025 katika kijiji cha Ruhembe ambapo yamebebwa na kauli mbiu isemayo “Chukua hatua sasa,Wewe, mimi, Jamii”.

Na Beatrice Majaliwa

Kuelekea katika Wiki ya Kichaa Cha Mbwa inayotarajiwa kuadhimishwa tarehe 28 Septemba 2025 wananchi wilayani Kilosa wametakiwa kuzingatia kanuni bora za ufugaji wa mbwa ikiwa ni pamoja na kuwapeleka kuwaogeshwa mara kwa mara na kuwapeleka kupata chanjo.
Wito huo ulitolewa na Afisa Mifugo Wilaya ya Kilosa Bwana David Shemweta alipokuwa akizungumza na Redio Jamii Kilosa katika Kipindi cha Ijue Halmashauri yako ambapo amesisitiza kuwa mbwa wanatakiwa kufugwa kama wanyama wengine wanavyofugwa majumbani hivyo nao wanatakiwa kuzingatiwa katika kila kitu kama vile kupata chanjo, kufungiwa na kufuliwa kwa wakati sahihi.

Afisa Mifugo Wilaya ya Kilosa Bwana David Shemweta

Shemweta ameongeza kwa kusema kuwa ndani ya wiki ya Kichaa cha Mbwa kuna mambo mbalimbali yanafanyika ikiwemo utoaji wa chanjo kwa mbwa sehemu mbalimbali na utoaji wa elimu ili wananchi wapate elimu zaidi kuhusiana na namna ya kujikinga na ugonjwa huu wa kichaa cha mbwa na pia kutumia njia sahihi za ufugaji wa mbwa.

Sauti ya Afisa Mifugo Wilaya ya Kilosa Bwana David Shemweta

Aidha Shemweta ameongeza kwa kusema kuwa wananchi wanapaswa kuchukua tahadhali mapema ili waweze kujikinga na ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwani ugonjwa huu ni hatari kama unakuwa haujawahiwa kutibiwa kwa mtu anapokuwa ameng’atwa au kuambukizwa ugonjwa huu na pia amesema kuwa ikitokea mtu ameng’atwa awahi hospitali kwa ajili ya kupata matibabu na mbwa achunguzwe kama ana kichaa au hana.

Sauti ya Afisa Mifugo Wilaya ya Kilosa Bwana David Shemweta

Sambamba na hayo ameongeza kwa kusema kuwa wafugaji wana fursa ya kufika ofisi ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya kushirikishana ujuzi na namna bora ya ufugaji kwani wataalamu wapo na wanapatikana na wanatoa ushirikiano mara tu mtu anapokuwa anahitaji hivyo ni vizuri wakajifunza na kuongeza ujuzi.