Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
11 September 2025, 2:20 pm

NGO’s hufanya kazi kwa kushirikiana na jamii na mara nyingi hupata ufadhili kutoka kwa wafadhili wa ndani au nje ya nchi kwa lengo la kusaidia maendeleo ya jamii katika nyanja mbalimbali kama vile afya, elimu, mazingira, haki za binadamu n.k., bila kuwa chini ya uongozi wa serikali.
Na Aloycia Mhina
Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) wilayani Kilosa yametakiwa kuanzisha miradi ya ndani itakayowawezesha kujiingizia mapato na kupunguza utegemezi kwa wafadhili ambao mara nyingi hubadilisha vipaumbele vyao na kuathiri utekelezaji wa miradi.
Wito huo ulitolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii ambaye pia ni Msajili Msaidizi wa NGOs wilayani hapa, Bw. Godwin Mbembela, alipokuwa akizungumza na Redio Jamii Kilosa katika kipindi cha Ijue Halmashauri Yako ambapo amesema kuwa mashirika hayo yanapaswa kuwa na mipango endelevu ya kujitegemea ili kufanikisha malengo yao hata pale wafadhili wanapojiondoa.
Bw Mbembela ameyataka mashirika hayo kushirikiana kwa karibu na watendaji wa kata katika maeneo wanayotekeleza miradi, sambamba na kutoa taarifa za fedha, bajeti na shughuli wanazofanya vijijini na kwamba kuna baadhi ya mashirika huanzisha vikundi vya kijamii bila taarifa rasmi kwa halmashauri.
Hadi sasa Wilaya ya Kilosa ina jumla ya mashirika 36 yasiyo ya kiserikali yaliyoandikishwa rasmi a usajili huo unafanyika kupitia mfumo wa kitaifa ambapo shirika linapaswa kuwa na katiba, barua ya maombi na malengo yanayozingatia mila na desturi za Kitanzania kabla ya kupata barua ya utambuzi kutoka halmashauri.