Radio Jamii Kilosa

OCS Kilosa ataka kudumisha amani kati ya wakulima na wafugaji

28 August 2025, 4:04 pm

Wakulima na wafugaji wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Kituo Kilosa OCS Mhina baada ya kuisha kwa mkutano wa hadhara uliofanyika kitongoji cha Rozi. Picha na Stamius Kyombo

Migogoro kati ya wakulima na wafugaji huondoa amani kwa kusababisha vurugu, uharibifu wa mali, chuki baina ya jamii, na hata vifo ambapo migogoro hii huathiri maisha, uchumi wa familia, na maendeleo ya kijamii kwa ujumla, hivyo kudumisha maelewano ni muhimu kwa usalama na ustawi wa wote.

Na Stamius Kyombo

Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Kilosa (OCS), Donati Mhina, ametoa wito kwa wakulima na wafugaji wilayani humo kudumisha amani, mshikamano na ushirikiano wa karibu ili kuondoa migogoro ya mara kwa mara kati ya pande hizo mbili. Kauli hiyo ameitoa Agosti 27, 2025, wakati akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Rozi, Kata ya Magomeni.

OCS Mhina amesema migogoro ya ardhi na matumizi ya maeneo baina ya wakulima na wafugaji imekuwa chanzo kikuu cha uvunjifu wa amani, hivyo kuna haja ya kuwa na umoja wa pamoja utakaosaidia kutambua changamoto mapema na kuzitatua kwa njia ya mazungumzo. Ametoa rai kwa wakulima na wafugaji kuunda vikundi vya usimamizi wa maeneo yao ili kudhibiti uingizaji holela wa mifugo mashambani.

Mkuu wa Kituo cha Polisi wilayani Kilosa Donati Mhina

Katika hotuba yake, Kamanda Mhina amewakumbusha wafugaji kuheshimu sheria kwa kutopeleka mifugo kwenye mashamba ya watu na kuacha tabia ya kuwatumikisha watoto wadogo kama wachungaji, akisisitiza kuwa hilo ni kinyume cha sheria ya Ajira ya Mwaka 2004. Pia ameshauri wafugaji kupunguza mifugo au kutafuta maeneo mbadala ya malisho, kutokana na maeneo yaliyopo kutotosheleza kwa idadi ya mifugo iliyopo kwa sasa.

Aidha, amewatahadharisha wananchi kuepuka vitendo vya rushwa vinavyoweza kuathiri haki katika utatuzi wa migogoro ya ardhi. Amewasihi kufuata sheria na kutumia njia sahihi za kisheria katika kutatua migogoro badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Sauti ya (OCS), Donati Mhina

Akiongea kwa niaba ya wakulima, Rabani Mgupala ameiomba serikali kuwatengea wafugaji maeneo mengine ya kufugia kwani yaliyopo kwa sasa hayatoshi kulisha idadi kubwa ya mifugo jambao ambalo linapelekea wafugaji kulisha kwenye mashamba yao.

Sauti ya mkulima Rabani Mgupala

Naye bwana Kitwilu ambaye ni mfugaji amewashauri wakulima kuwatambua wafugaji wenye tabia za kulisha mashamba yao ili hatua za kisheria zichukuliwe huku akibainisha wazi kuwa si wafugaji wote wenye tabia za kuchungia mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima.

Sauti ya mfugaji Bw Kitwilu
Baadhi ya wananchi wakifuatilia mkutano huo wa hadhara