Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
27 August 2025, 8:24 pm

Mikopo ya asilimia 10 ni fedha zinazotolewa na Halmashauri zote nchini kwa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu ambapo kila Halmashauri hutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani—asilimia 4 kwa wanawake, 4 kwa vijana, na 2 kwa watu wenye ulemavu na mikopo hiyo haina riba, hulenga kuinua maisha ya wananchi kiuchumi na kuendeleza shughuli za uzalishaji kupitia vikundi vya ujasiriamali. Mikopo hutolewa kwa masharti ya kurejeshwa ili vikundi vingine vinufaike pia.
Na Asha Madohola
Vikundi 38 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa leo Agosti 27, 2025, wamekabidhiwa mikopo yenye thamani ya shilingi 541,310,000 kupitia mpango wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Hafla ya utoaji wa mikopo hiyo imefanyika katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, aliyesaini hundi ya mikopo hiyo kwa niaba ya serikali.

Wakizungumza kwa niaba ya wanavikundi wengine, Bi Halima Said kutoka Magole, ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwaamini wananchi na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo hiyo isiyo na riba huku akiahidi kuwa fedha hizo zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kurudishwa kwa wakati.


Kwa upande wake, Andrew Mtikita, Meneja Huduma kwa Mteja kutoka taasisi ya kifedha NMB iliyoshirikiana na Halmashauri, ametoa rai kwa wanufaika kuwa na nidhamu ya kifedha, kupanga matumizi ya mkopo kwa umakini, na kuhakikisha wanatimiza malengo ya biashara zao na kwamba benki ipo tayari kushirikiana nao kuwapa elimu ya fedha na mbinu bora za uendeshaji wa biashara.

Afisa wa TAKUKURU Wilaya ya Kilosa, Elias Masila, alitumia nafasi hiyo kukumbusha kuwa fedha hizo ni mali ya umma, hivyo ni lazima zitumike kwa uadilifu na kusema TAKUKURU itafuatilia matumizi ya mikopo hiyo na kuchukua hatua stahiki endapo kutabainika matumizi mabaya au ubadhirifu wowote na kwamba jukumu la kila mnufaika ni kuhakikisha fedha hizo zinaleta matokeo chanya katika jamii.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kurudisha mikopo hiyo kwa wananchi, huku akiwasisitiza wanufaika kutumia fedha hizo kwenye shughuli za kiuchumi badala ya starehe.
Amewakumbusha kuwa urejeshaji wa fedha hizo kwa wakati utawasaidia kupata mikopo mikubwa zaidi siku za usoni na kusaidia vikundi vingine ambavyo bado havijanufaika kutokana na uhitaji mkubwa uliopo.

Awali akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilosa, Bi Beatrice Mwinuka kabla ya kumkaribisha Mkuu wa wilaya ya Kilosa alisisitiza pia umuhimu wa urejeshaji ili kuongeza wigo wa wanufaika wa mkopo huo.
