Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
21 August 2025, 1:37 pm

Chakula shuleni ni muhimu kwa maendeleo ya afya na elimu ya mwanafunzi. Huchangia kuongeza nguvu na uwezo wa kujifunza, hupunguza utoro, na huimarisha mahudhurio ya wanafunzi darasani na lishe bora pia huongeza uwezo wa kufikiri, umakini na utendaji wa mwanafunzi.
Na Asha Madohola
Katika kikao cha utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa robo ya nne (Aprili–Juni 2025) kilichofanyika Agosti 20 wilayani Kilosa, Mkuu wa Wilaya Mhe Shaka Hamdu Shaka alitoa wito kwa viongozi na watendaji wa kata zote kuongeza juhudi katika kuhamasisha wazazi na walezi kuchangia chakula shuleni.
Kikao hicho kimewakutanisha watendaji wa kata, wataalamu wa lishe, na viongozi mbalimbali kujadili maendeleo ya lishe mashuleni.

Taarifa iliyotolewa imeonesha kuwa baadhi ya kata hazijafanya vizuri katika utoaji wa chakula mashuleni kutokana na changamoto ya viongozi kushindwa kuwashawishi wananchi kuona umuhimu wa kuchangia chakula kwa watoto wao.
Mkuu wa Wilaya amesema suala la lishe bora shuleni ni la lazima kwa maendeleo ya elimu na afya za watoto na amewataka wakuu wa shule kuhakikisha chakula kinatolewa kwa usalama na kuwa na virutubisho stahiki.

Afisa Lishe Wilaya ya Kilosa, Elisha Kingu, akitoa taarifa ya viashiria vya lishe, amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaopata chakula shuleni kutoka asilimia 64.03 katika robo ya tatu hadi asilimia 84.87 kwa robo ya nne, jambo linaloonesha mafanikio ya juhudi za uhamasishaji. Hata hivyo, ameongeza kuwa bado kunahitajika juhudi zaidi kuhakikisha shule zote zinatoa chakula.
Kwa upande wake Afisa Lishe Bi Salha amesema lishe bora ni msingi wa afya na maendeleo ya mtoto, hivyo ni muhimu wazazi kushirikiana na shule na viongozi kuhakikisha watoto wanapata mlo kamili shuleni. Amesema chakula shuleni si jukumu la Serikali pekee bali ni wajibu wa pamoja wa jamii nzima.

Aidha, Mtendaji wa Kata ya Masanze kwa niaba ya watendaji kata amesema wamepokea maelekezo hayo na wako tayari kuyaleta kwenye vikao vya vijiji ili wazazi waelimishwe juu ya umuhimu wa kuchangia chakula. Wazazi wengi, amesema, huona ni mzigo lakini ukweli ni kwamba ni uwekezaji wa moja kwa moja kwa maendeleo ya watoto wao.
Afisa Kilimo Bi Zena Omary amewataka watendaji kushirikiana na maafisa kilimo katika kuanzisha bustani shuleni kwa shule zisizo na uwezo wa kifedha. Amesema njia hiyo itasaidia kupatikana kwa mboga na mazao ya chakula shuleni kwa gharama nafuu, huku ikiwajengea wanafunzi uelewa wa kilimo cha bustani.
