Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
19 August 2025, 11:38 pm

Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) ni mradi wa Serikali ya Tanzania unaolenga kusaidia kaya zenye hali duni za kiuchumi kwa kuwapatia ruzuku ya fedha, fursa za ajira za muda na kuwajengea uwezo wa kujitegemea na mradi huu umejikita katika kuboresha maisha ya walengwa kupitia miradi ya kijamii, uundaji wa vikundi vya akiba, na kusaidia mahitaji muhimu kama elimu, afya na lishe.
Na Asha Madohola
Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) wilayani Kilosa, wameeleza mafanikio makubwa waliopata kupitia mpango huo wa miaka kumi, huku wakiiomba Serikali kuendeleza msaada huo kutokana na mahitaji yanayoendelea kuwapo kwenye jamii.

Wakizungumza katika Kijiji cha Rudewa kwa nyakati tofauti akiwemo Omary Somvi, wanufaika hao wamesema TASAF imekuwa mkombozi wa maisha yao kwa kuwasaidia kupata chakula, kupeleka watoto shule, kujenga makazi bora na hata kuanzisha biashara ndogondogo.

Hata hivyo akizungumza mnufaika Sikudhani Kibwana alitoa wito kwa Serikali kuangalia uwezekano wa kuanzisha awamu mpya ya TASAF, wakisema bado kuna makundi mengi yenye uhitaji mkubwa wa msaada na uwezeshaji kwa mustakabali bora wa maisha.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Rudewa, Masudi Msabaha, amesema mafanikio ya mradi huo yameonekana wazi kwa wanavijiji, ambapo baadhi yao sasa wana uwezo wa kujitegemea.

Kwa upande wake, Mwezeshaji wa TASAF ngazi ya Wilaya, Bi. Mwanaidi Rajabu, amesema tangu kuanza kwa mpango huo mwaka 2013, kaya zaidi ya 10,000 zimeandikishwa na wanufaika zaidi ya 35,000 wamepata ruzuku pamoja na kushiriki katika vikundi vya kuweka akiba na kuongeza kipato.
Naye Mratibu wa TASAF wilayani Kilosa, Dedan Maube, amesema malipo yanayoendelea ni ya mwisho kwa awamu hii, na walengwa wamepatiwa bonasi ili kuendeleza shughuli za kiuchumi.
Hata hivyo amewahimiza wanufaika kutumia vizuri fedha hizo kwa maendeleo ya familia na jamii zao.
Dirisha la malipo kwa wanufaika wa mradi wa Tasaf kwa siku ya kwanza ambalo limeanza 19 Agosti 2025 limefanyika katika vijiji vya kata za Magomeni, Kasiki, Mkwatani, Chanzuru, Mabwerebwere, Kimamba A&B, Parakuyo, Madoto, Rudewa, na Mvumi.

