Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
26 July 2025, 11:15 am

Mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa vijana wanawake na watu wenye ulemavu inafanya kazi kama mfuko unaozunguka ambapo mikopo hiyo inakusudiwa kuimarisha shughuli zinazowaingizia kipato wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wasio na ajira rasmi na hivyo kuboresha maisha yao kwa ujumla.
Na Aloycia Mhina
Wana vikundi vilivyokopeshwa fedha kutoka asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa wametakiwa kuhakikisha wanazitumia fedha hizo kwa malengo ya kuendeleza biashara zao kama walivyopanga awali, badala ya kugawana miongoni mwao.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii ambaye pia ni Mratibu wa Mikopo ya Asilimia Kumi, Ndg William Jonathan Mlay, wakati akizungumza na Redio Jamii Kilosa.
Mlay amesema mikopo hiyo hutolewa kwa makubaliano ya kisheria na kusisitiza kuwa ni wajibu wa wanavikundi kutekeleza masharti ya mikataba yao ili kufanikisha malengo ya serikali ya kuwawezesha kiuchumi.
Aidha, Mlay alisema kuwa baadhi ya vikundi vimekuwa vikikosea kwa kugawana fedha hizo badala ya kuziwekeza katika biashara walizoziandika kwenye maandiko yao ya mradi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na linaweza kuwakosesha fursa za mikopo ya baadaye.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Elistone Daniel Elibahati, alieleza kuwa mikopo hiyo haina riba na hutolewa kwa vikundi vyenye sifa, akiwataka wananchi wenye nia ya kukopa kuwasiliana na maafisa wa maendeleo waliopo katika vijiji, vitongoji na kata ili kupata mwongozo.
Hata hivyo alisisitiza umuhimu wa kulipa marejesho kwa wakati ili vikundi viendelee kukopesheka na kutoa nafasi kwa wengine kunufaika.