Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
4 July 2025, 10:52 pm

Wananchi na wawekezaji wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo wilayani Kilosa, ikiwemo kilimo, utalii na viwanda, ili kuchochea uchumi na maendeleo ya Taifa.
Na Beatrice Majaliwa
Wananchi ndani na nje ya Wilaya ya Kilosa wametakiwa kutumia kikamilifu fursa zilizopo za uwekezaji ili kuimarisha uchumi na kujiletea maendeleo.
Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, wakati wa kikao cha Baraza la Biashara kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.
Mhe. Shaka amesema Wilaya hiyo imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ambazo ni fursa za kiuchumi kwa wawekezaji, zikiwemo sekta za utalii, kilimo, madini, mazingira na viwanda.
Amehimiza wadau wa sekta binafsi kushirikiana na serikali ya Wilaya hiyo ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Wilaya ya Kilosa, Bw. Edward Mapile, alisema kuwa Baraza la Biashara ni jukwaa muhimu linalowawezesha sekta binafsi na serikali kujadiliana, kubadilishana taarifa za maendeleo pamoja na kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya kiuchumi wilayani hapa.
Bw. Mapile ameongeza kuwa miundombinu iliyopo, ikiwemo reli ya kisasa ya SGR, imefungua milango zaidi kwa wawekezaji, hivyo ni muhimu kwa wafanyabiashara na wawekezaji kutumia fursa hiyo kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.