Radio Jamii Kilosa

Viongozi Kilosa wakumbushwa wajibu wao

3 July 2025, 3:51 pm

Mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe Shaka Hamdu Shaka akiwa katika kikao na watendaji kata na vijiji. Picha na Beatrice Majaliwa

Uvunaji wa misitu ni mchakato wa kuvuna mazao ya misitu kama magogo, kuni, na mkaa kwa kufuata taratibu rasmi na mipango ya matumizi bora ya ardhi. Uvunaji huo unapaswa kuwa endelevu ili kuepuka uharibifu wa mazingira.

Na Beatrice Majaliwa

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, amewataka viongozi wa kata na vijiji kushirikiana kwa dhati katika kutekeleza majukumu yao ya maendeleo kwa maslahi ya wananchi, bila kutanguliza maslahi binafsi.

Akizungumza, katika kikao cha tathmini ya uvunaji wa mazao ya misitu wilayani humo, Mhe. Shaka alisema kuwa viongozi wamepewa dhamana ya kuwatumikia wananchi kwa haki na uwazi, na kusisitiza kuwa kushindwa kushirikiana kunarudisha nyuma jitihada za maendeleo.

Mhe. Shaka ameonya dhidi ya vitendo vya rushwa na upendeleo, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kusimamia sheria, kanuni na taratibu zilizopo kwa kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali za misitu kwa manufaa ya wote.

Mhifadhi Misitu Bi Hilda Mwalongo akizungumzia uvunaji misitu

Kwa upande wake, Mhifadhi Misitu wa Wilaya ya Kilosa, Bi. Hilda R. Mwalongo, amesema uvunaji wa mazao ya misitu unasaidia katika kuongeza mapato ya vijiji na serikali kwa ujumla, hivyo unapaswa kufanyika kwa kufuata utaratibu na mipango madhubuti ili kulinda mazingira.

Sauti ya Bi Hilda Mwalongo akizungumzia kuhusu kuvuna misitu

Nao viongozi wa vijiji, akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji cha Chabima, Julius Magungu, walisema wamepata uelewa mkubwa juu ya umuhimu wa uhifadhi wa misitu, na kuahidi kusimamia kikamilifu maeneo waliyopewa kwa kuzingatia matumizi bora ya ardhi na uvunaji endelevu.

Sauti ya Mwenyekiti wa kitongoji cha Chabima Julius Magungu akizungumza