Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
25 May 2025, 4:05 pm

Serikali inaendelea kuwekeza katika elimu ya lishe, na kuongeza upatikanaji wa vyakula vyenye virutubisho muhimu kwa mama na mtoto na lengo ni kuhakikisha jamii inapata lishe bora na afya njema kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Na Asha Madohola
Kata ya Berega wilayani Kilosa 24 Mei imefanya Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji kwa kushirikisha vijiji vyake vinne, ambapo wananchi walijifunza kwa vitendo namna ya kuandaa uji wa lishe bora ambapo watoa huduma za afya ngazi ya jamii (CHW) waliandaa uji huo na kutoa elimu juu ya umuhimu wa makundi sita ya chakula katika maandalizi ya lishe kwa watoto.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Berega Marry Fungo alisema siku ya afya na lishe kijiji imefanyika katika vijiji vinne umuhimu wa kuendelea kushirikiana na wataalamu wa afya na viongozi wa kijiji katika kuhakikisha elimu ya lishe inawafikia wananchi wote.

Aidha Afisa Lishe wa Wilaya alitembelea baadhi ya vijiji na kutoa elimu ya kina kuhusu lishe bora kwa watoto chini ya miaka mitano, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha huku akisisitiza kuwa ulaji wa makundi sita ya chakula ni muhimu ili kupata virutubisho vya kutosha ili kujenga afya imara kwa mama na mtoto, na kuzuia matatizo ya udumavu, ukondefu na uzito pungufu.

Kaimu Mganga Mkuu Prosper Mlonge naye alihimiza elimu hiyo iendelee kutolewa kwa wananchi kwa kutumia mikutano ya kijiji, ili ujumbe uwafikie wengi kwa wakati mmoja. Amesema ushirikiano kati ya wataalamu wa afya na viongozi wa kijiji ni muhimu katika kufanikisha afua za lishe.

Wananchi waliopata elimu hiyo akiwemo Bi Magreth Maranda walionesha kufurahishwa na maarifa mapya waliyojifunza, huku wakiahidi kuyatumia katika familia zao kwa lengo la kuboresha afya za watoto na kina mama katika jamii yao.
