Wilaya ya Kilosa imeanza mchakato wa bajeti ya kuboresha lishe
6 December 2024, 8:16 pm
Wito umetolewa kwa serikali kutoa fedha kwa wakati na kwa kiwango kinachohitajika, huku jamii ikihamasishwa kuchukua jukumu kubwa katika kuhakikisha kila kaya inazingatia lishe bora kwa ajili ya afya na ustawi wa watoto.
Na. Asha Rashid Madohola
Wilaya ya Kilosa imeanza rasmi maandalizi ya bajeti ya afua za lishe kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa na lengo la kuboresha hali ya lishe kwa wananchi, hasa watoto, ambao kwa sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa za ukondefu na utapiamlo.
Kikao kazi cha awali cha kupanga bajeti hiyo kimefanyika leo katika ukumbi wa Maktaba uliopo katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa ambapo kikao hicho kimewakutanisha wataalamu wa idara mbalimbali,viongozi wa halmashauri, waliokusudia kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha lishe na kuhakikisha fedha za bajeti zinatengwa kwa ufanisi.
Akifungua kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Ndg. Alto Kimbiye, alitoa tahadhari juu ya hali mbaya ya lishe wilayani humo ambapo alieleza kuwa ukosefu wa lishe bora kwa wananchi, hususan watoto, umekuwa changamoto kubwa inayochangia udumavu, utapiamlo, na kushuka kwa mahudhurio shuleni.
Aidha alisema kuwa changamoto kubwa ni ukosefu wa chakula cha mchana shuleni na uelewa mdogo wa lishe bora kwa familia nyingi na kwamba halmashauri inalenga kutumia kikao hicho kuanzisha mwelekeo mpya wa maendeleo kupitia lishe bora.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Mkoa wa Morogoro, Bi. Salome Magembe, aliwasilisha takwimu za kushtua zinazodhihirisha hali mbaya ya lishe wilayani Kilosa ambapo alisema watoto wengi wilayani hapa wanakabiliwa na ukondefu mkali na utapiamlo, hali ambayo inatokana na changamoto za kiuchumi, kijamii, na ukosefu wa chakula cha mchana shuleni.
“Takwimu zinaonyesha kuwa ukosefu wa chakula cha mchana shuleni umeathiri kwa kiwango kikubwa maendeleo ya watoto kimwili na kiakili. Tunaiomba serikali kuhakikisha kwamba bajeti zinazotengwa kwa ajili ya lishe zinatolewa kwa wakati na kwa kiwango kilichoombwa, ili kuimarisha afua za lishe na kupunguza changamoto hizi,” alisema Magembe.
Naye Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Ndg. Npela Kwidika, aliongeza kwamba mipango ya kifedha itakuwa msingi wa mafanikio ya mpango wa lishe wilayani humo na kwamba kikao hicho kinatoa fursa kwa halmashauri kupanga bajeti yenye ufanisi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
“Kama idara ya fedha, tutatoa kipaumbele kwa bajeti ya lishe kwa sababu tunaamini kuwa afya bora ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Kupitia kikao hiki, tunatarajia kuweka msingi wa mageuzi makubwa ambayo yatafanikisha mabadiliko chanya katika hali ya lishe ya watoto na jamii nzima ya Kilosa,” alisema Kwidika.
Afisa Lishe wa Wilaya ya Kilosa, Ndg. Elisha Kingu, alieleza kuwa bajeti ya awali ya shilingi milioni 140 imependekezwa kushughulikia changamoto za lishe katika wilaya hiyo na alifafanua kuwa fedha hizo zitatumika kuboresha elimu ya lishe kwa jamii, kuimarisha huduma za lishe katika vituo vya afya, na kuhakikisha watoto shuleni wanapata chakula cha mchana.
“Bajeti hii tumeipanga kwa umakini mkubwa ili kufanikisha malengo ya kupunguza ukondefu na kuongeza uelewa wa lishe bora kwa kila familia na tunataka kuhakikisha kuwa kila mtoto, kila mzazi, na kila kaya wanajua umuhimu wa lishe bora kwa maendeleo yao na ya jamii kwa ujumla na kwamba elimu ya lishe itakuwa kipaumbele kikubwa ili kuhakikisha jamii inashiriki kikamilifu katika kuboresha hali ya lisheā€¯ alisema Kingu.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa wajumbe wote kukubaliana kuwa ushirikiano kati ya serikali na jamii ni muhimu kwa mafanikio ya mpango huo ambapo wajumbe walisisitiza kuwa lishe bora ni msingi wa maendeleo endelevu ya wilaya na taifa kwa ujumla.