Radio Jamii Kilosa

Viongozi wa serikali za mitaa Kilosa waapishwa, watakiwa kuwa waadilifu

30 November 2024, 12:21 am

Kushoto ni Afsa Utumishi wilaya ya Kilosa Ndg Betuely Joseph Ruhega akiwa na Hakimu Mkazi Mhe Martin Morris Cyprian akizungumza katika hafla ya kula kiapo kwa viongozi. Picha na Asha Mado

Wilayani Kilosa, viongozi wapya wa serikali za mitaa waliopatikana kupitia uchaguzi uliofanyika Novemba 27 na 28 mwaka huu wameapishwa rasmi tarehe 29 Novemba 2024 .

Viongozi hao, wakiwemo wenyeviti wa vijiji, wenyeviti wa vitongoji, wajumbe wa viti maalum, na wajumbe wa kundi mchanganyiko, wamekula kiapo katika hafla zilizofanyika kwenye kata mbalimbali za wilaya hiyo, ikiwemo Tindiga, Masanze, Zombo, Ulaya, Mhenda, na Kisanga.

Hafla hiyo ilifanyika chini ya usimamizi wa Mhe. Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Kilosa, Martin Morris Cyprian ambapo akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Afisa Utumishi wa Halmashauri hiyo, Ndg Betuely Joseph Ruhega, amewakumbusha viongozi hao umuhimu wa kutambua dhamana waliyopewa na wananchi na kuwataka viongozi hao kuonyesha uadilifu, uwajibikaji, na kutanguliza maslahi ya jamii katika kila hatua ya uongozi wao.

Sauti ya Afsa Utumishi Ruhega akizungumza

Aidha Ruhega alisisitiza kuwa viongozi hao ni watumishi wa umma, hivyo wanapaswa kusimamia miradi yote ya maendeleo, kuhakikisha mapato ya vijiji yanakusanywa na kuwekwa benki, na viapo hivyo vya utii vikawe tija kwa wananchi.

“Tunawategemea viongozi hawa kuwa daraja kati ya serikali na wananchi. Simamieni miradi ya maendeleo kwa weledi, hakikisheni mapato yanakusanywa kwa uwazi, na jitahidini kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na juhudi za maendeleo katika vijiji vyenu” alisema Ruhega.

Sauti ya Ruhega akizungumza

Baadhi ya Watendaji wa kata waliokuwepo katika hafla hizo nao walitoa wito kwa viongozi hao kuhakikisha wanachukua hatua zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi waliowachagua.

Sauti Afsa Mtendaji Ulaya akizungumza
Viongozi wakila kiapo

Mhe. Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Kilosa, Martin Cyprian, ambaye alisimamia kiapo hicho, aliwakumbusha viongozi hao kuwa kiapo walichokula si jambo la kawaida bali ni ahadi rasmi inayowalazimu kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na kwamba kushindwa kutimiza ahadi hizo ni sawa na kukosa kuheshimu dhamana ya wananchi.

Hafla za kuapishwa kwa viongozi hao ni mwanzo wa safari mpya ya maendeleo katika Wilaya ya Kilosa ambapo Halmashauri ya Wilaya hiyo inawataka viongozi hao kushirikiana na wananchi ili kufanikisha malengo ya maendeleo.