Radio Jamii Kilosa

Watumishi wa afya Kilosa wapewa nondo kubaini ukondefu, udumavu kwa watoto

15 November 2024, 2:00 pm

Afsa lishe akimpima mtoto urefu ili kubaini hali ya ukuaji wake. Picha na Mbaraka

Serikali inaendelea kupambana na changamoto zinazowakabili watoto chini ya miaka miwili ambao wamekuja wakikabiliwa na ukondefu mkali ama utapiamulo pamoja na udumavu kwa kutoa elimu kwa watumishi wa afya.

Na Asha Rashid Madohola

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Lishe, Ndugu Elisha Kingu, alitoa mafunzo muhimu kwa watumishi wa afya kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya kupima na kufuatilia hali ya lishe ya watoto.

Mafunzo hayo yalifanyika katika Kituo cha Afya Msange, Zahanati ya Kisanga, na Zahanati ya Ihombwe ambapo Afsa Lishe Kingu alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kwamba watumishi wanajua namna ya kutumia vibao vya kupimia urefu, maarufu kama Length board, pamoja na kanda za MUAC na kujaza taarifa muhimu kwenye vitabu vya takwimu za watoto.

Mtoto akipimwa urefu ili kufahamu kimo cha ukuaji wake ( udumavu)

“Kwa mujibu wa Ndugu Kingu, vifaa hivi vikitumiwa ipasavyo, vinaweza kusaidia kubaini mapema kama mtoto anakua vizuri au anahitaji msaada wa matibabu na kupitia vifaa hivyo, wahudumu wa afya wanaweza kuchukua hatua za haraka kutoa rufaa au matibabu kwa watoto wanaokabiliwa na tatizo la lishe” alieza Afsa Lishe Kingu.

Aidha Afsa lishe Kingu aliweka wazi kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za wilaya ya Kilosa kuimarisha afya za watoto na kupambana na changamoto za lishe duni huku akitoa wito kwa watumishi wa afya kuhakikisha wanatumia elimu na ujuzi walioupata ili kuwasaidia watoto kupata makuzi bora na kuepuka madhara ya lishe duni.

Wakizungumza baadhi ya Watumishi walioshiriki katika mafunzo hayo akiwemo Denis Charles na St. Anisia Mzeru walielezea furaha yao na kupongeza jitihada hizo za Kitengo cha Lishe wilayani Kilosa ambapo wengi wao wamekiri kuwa mafunzo hayo yameongeza maarifa yao kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya kupimia hali ya lishe na kuwasaidia kufahamu hatua za kuchukua mara baada ya kubaini matatizo ya ukuaji kwa watoto.

Hata hivyo, watumishi hao walisema changamoto zilizokuwepo hapo awali ilikuwa ni upungufu wa ujuzi katika ujazaji sahihi wa takwimu hizo, ambapo makosa kidogo kwenye taarifa hizo yanaweza kuathiri huduma zinazotolewa kwa watoto na hata mipango ya kitaifa ya afya ya lishe na wamekiri kuwa walikuwa wakipata changamoto katika kupima watoto kwa usahihi kabla ya mafunzo hayo, lakini sasa wana imani kuwa watakuwa na uwezo wa kuwahudumia watoto kwa viwango vya ju