Wananchi Mbumi watakiwa kuacha kutupa uchafu kwenye mifereji
10 March 2024, 1:05 am
Katika kuhakikisha wananchi wanaishi kwa usalama kipindi chote cha kiangazi na masika serikali imeamua kuwajenge mifereji ambayo itarahisha upitisha maji msimu wa mvua a na kupunguza maji kusambaa kwenye makazi ya watu na kuleta maafa.
Na Asha Madohola
Wananchi waishio katika kata Mbumi wilayani Kilosa wameishukuru serikali kwa kuwajengea mifereji ya kupitisha maji kipindi cha mvua kwani imekuwa mkombozi kwao kwa kuwaepusha na adha ya mafuriko iliyokuwa ikiwakumba na kuwataka wananchi wenzao washirikiane kuitunza
Wakizungumza katika ziara ya Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof Palamagamba Kabudi aliyefika kukabidhi mradi wa ujenzi wa mfereji wa mita 450 kwa wakandarasi wa kampuni ya Kupala Works ambao wanautekeleza kwa awamu ya pili baada ya kumaliza awamu ya kwanza kwa wakati na ubora.
Licha ya wananchi hapo kushukuru serikali lakini Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof Palamagamba Kabudi aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuitunza mifereji hiyo kwa kuacha kutupa uchafu na kutapisha maji ambayo itapelekea mifereji kujaa na kuziba na kushindwa kupelekea maji nakuleta maafa, hivyo wasafishe mitaro iliyopita mbele ya nyumba zao.
“Kwa hali niliyoanza kuiona hapa si nzuri mitaro imejaa magogo, machupa na mchanga na kwa kuwa uchafu huu unaendelea nitakuja kuisafisha mifereji hii kwa mikono yangu bila ya kuvaa glovu ili mjue kama sipendi uchafu na wala sitakufa na kipindupindu Mungu atanilinda” alisema Prof Kabudi.
Aidha Mbunge Prof Kabudi alisema kuwa eneo la Mbumi limekua likiathiriwa na mafuriko mara kwa mara lakini kwa ujenzi wa mradi mfereji awamu ya kwanza uliwanusuru na awamu ya pili wamepatiwa milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa mfereji wa mita 450 na kuwataka wakandarasi kumaliza mradi kwa wakati ili wananchi wanufaike.
Meneja wa Tarura wilaya ya Kilosa Winston Mnyaga alisema kuwa anamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha za dharula zaidi ya shilingi bilioni 1.3 zimetolewa wilayani Kilosa kwa ajili ya kujenga na kurekebisha sehemu korofi zilizoathirika kipindi cha mvua za elnino na kukamilika kwake wananchi wataishi kwa amani msimu wa mvua.
Kwa upande wake mkandarasi Bi Mary Sanga ambaye ndiye Mkurugenzi wa ufundi katika kampuni hiyo ya Kupala amesema hiyo ni kazi ya dharula hivyo watajitahidi kukamilisha kwa wakati ili mvua zitapoanza kunyesha wananchi wasipate maafa ya mafuriko.