Wafanyabiashara waridhia tozo ya shilingi 50,000.
13 February 2021, 5:28 pm
Wafanyabiashara waliopanga katika vibanda vinavyomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa vilivyoko katika kata ya Kasiki maeneo ya uhindini wamekubali kulipa tozo ya shilingi 50,000 kwa mwezi kwa kibanda hadi hapo vitakapofanyika vikao vya kisheria mara baada ya mwaka wa fedha 2020/2021 kuisha.
Makubaliano hayo yamefanyika Februari 13 mwaka huu katika kikao cha pamoja baina ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale na wafanyabiashara hao ambapo ametolea ufafanuzi wa kina tozo halali kwa kibanda kwa mwezi ni 50,000, ambayo ilipitishwa kihalali katika vikao vya kisheria na kwamba tozo hiyo itadumu hadi mwaka wa fedha 2020/2021 utapoisha ambapo pia vikao hivyo vina mamalaka ya kushusha ama kupandisha tozo hiyo kwa kadri itakavyoamua na kuridhiwa na baraza la madiwani.
Itakumbukwa siku chache zilizopita wafanyabiashara hao waliopanga katika vibanda hivyo walifunga vibanda zaidi ya 200 wakiishinikiza Halmashauri kutoza shilingi 30,000 kwa kibanda kwa mwezi huku wakidai baraza la madiwani la Februari 6 mwaka 2020 lilipitisha tozo hizo.
Mwambambale amesema tozo ya shilingi 30,000 ni hoja iliyoibuka katika kikao cha kawaida cha baraza la kawaida la madiwani Februari 6 mwaka 2020 ambapo kwa mujibu wa sheria na kanuni haiwezi kuingia katika utekelezaji kwa kuwa haikufuata kanuni, taratibu na sheria ili kupata nguvu kuingia katika utekelezaji.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara Kilosa Joshua Charuza amesema wameridhia tozo ya shilingi 50,000 kwa kibanda kwa mwezi mpaka mabadiliko yatakapofanyika kwa kufuata utaratibu wa kisheria huku akitoa wito kwa wafanyabiashara kulipa kodi hiyo na nyingine ili kuleta maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.
Naye mfanyabiashara Fadhili Kondo amelaani vikali upotoshwaji uliofanywa na baadhi ya madiwani kwa wafanyabiashara wa kuwaaminisha kuwa tozo mya 30,000 ni halali huku wakijua kuwa tozo hiyo haipo kisheria na hakuna mahali popote ilipopitishwa hivyo waache kuwachonganisha wafanyabiashara na viongozi wa Halmashauri kwani wanampa wakati mgumu Mkurugenzi kutimiza majukumu yake katika kuiletea maendeleo Kilosa.