Shule ya Sekondari Mazinyungu yajipanga Kuizika Sifuri 2021.
2 February 2021, 11:20 am
Wanafunzi wa kidato cha nne shule ya Sekondari Mazinyungu Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wemejipanga kuzika Daraja sifuri ili isionekane shuleni hapo katika matokeo ya Kidato cha nne mwaka 2021.
Wakizungumza Januari 29 mwaka huu katika kikao mkakati cha kuzika sifuri wanafunzi hao wamesema kuwa ili kufuta sifuri katika shule hiyo wameweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujisimamiana wenyewe kinidhamu , kutengeneza makundi ya kujisomea ,kujijenga kimaadili na kuwa na ushirikiano katika kila somo ili kuweza kujadili mada mbalimbali zitakazofundishwa.
Naye Mkuu wa shule ya Sekondari Mazinyungu Ngamba Manegese amesema kuwa shule imezidi kupiga hatua kutoka asilimia 63 ya mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 94 ya mwaka 2020 ambapo ameongeza kuwa kwa muelekeo huo wameweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupanga , kusimamia, kufuatilia na kufanya tathimini ya mipango waliyo jiwekea katika kutekeleza mikakati ya Elimu kama maelekezo ya Serikali kadri yatakavyotolewa.
Amesema kuwa kwa sasa shule imeweka kaulimbiu ya KAIZIKE SIFURI ISIONEKANE MAZINYUNGU ambapo amesema kama shule teyari wameandaa mazingira mazuri ya kujifunzia ikiwa ni pamoja na kuweka taa kutenga madarasa ya makambi ikiwa ni pamoja na walimu kutoa majaribio ya kushtukiza .
Hata hivyo amesema anamshukuru Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Elimu Sekondari Wilaya kwa hamasa waliyokuwa wakitoa na maelekezo mbalimbali shuleni hapo ikiwa ni pamoja na kuanzisha kwa makambi ya wanafunzi ambayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kufanya vizuri.