Wakuu wa shule watakiwa kumaliza Ujenzi wa Madarasa Kilosa -Mgoyi.
16 January 2021, 7:38 pm
Katika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa kuwa ifikapo tarehe 15 Januari miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa iwe imekamilika Mkuu Wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ametembelea miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule mbalimbali ikiwemo shule za sekondari Mkulo, Kilosa, Dumila, Magubike, Magole na Dakawa Mazoezi ili kujiridhisha na utendaji kazi wa miradi hiyo.
Ziara hiyo imefanyika hivi karibuni ambapo Mgoyi amesikitishwa na baadhi ya shule za sekondari kutotekeleza miradi kwa wakati kwani muda wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kuripoti umewadia na agizo la Waziri Mkuu ni ifikapo Januari 15 miradi yote ya ujenzi wa vyumba vya madarasa iwe imekamilika ambapo ametoa siku 3 hadi kufikia Januari 17 wawe wamekamilisha miradi na kukabidhi ili wanafunzi wa kidato cha kwanza waweze kuripoti mashuleni.
Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari Paula Nkane amewaasa wakuu wa shule hizo pamoja na wasimamizi wa miradi kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi kwa kufuata sheria na miongozo waliyowekewa na waendelee kuwahamasisha wananchi wajitokeza katika kushiriki ujenzi wa madarasa kwani wahusika ni watoto wao, hivyo amewasisitiza maafisa watendaji kupiga la mgambo ili wananchi wajitokeze kwa wingi kuongeza nguvu kazi au kuchangia pesa zitakazowezesha mafundi kulipwa ili kazi ifanyike kwa kasi zaidi huku akiwapongeza wakuu wa shule waliotekeleza agizo hilo kwa wakati.