Huheso FM

Serikali ya Mtaa yaifukuza SAMBA MICROFINANCE kwa kuwaumiza wananchi

February 26, 2025, 5:31 pm

Picha ya mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Nyihogo, Idd Mitimingi wakati akizungumzia hatua walizochukua dhidi ya SAMBA MICROFINANCE

“Hawa akina mama walikopa mwezi Januari tarehe 30, 2025 walitakiwa kufanya marejesho ya mkopo mwezi March 01, 2025 lakini kabla hata muda wa kurudisha haujafika wamepeleka hela wanakataliwa wanapigwa penati ya mara mbili ya fedha ambayo walitakiwa kurejesha hii sio haki hii kampuni waondoke mtaani kwangu kwa sababu wanaumiza wananchi wangu”

Na Paschal Malulu

Serikali ya Mtaa wa Nyihogo, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga imeitaka kampuni ya mikopo ya SAMBA MICROFINANCE kuondoka katika Mtaa huo baada ya kubainika kuwaumiza wananchi wanaokopa kwenye kampuni hiyo.

Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa huo Iddi Mitimingi amesema kuwa wamefikia hatua hiyo mara baada ya akina mama wawili kufika ofisini kwake wakilalamikia kubambikiwa riba ya mkopo waliochukua ingawa wapo ndani ya muda wa kurejesha fedha waliyokopa.

Bwana Mitimingi amesema akina mama hao walikopa Januari 30, 2025 kwa kiwango tofauti mmoja alikopa kiasi cha shilingi Elfu Themanini (80,000) na alipaswa kurejesha shilingi laki moja (100,000) huku mwingine akikopa shilingi Elfu tisini (90,000) akitakiwa kurejesha shilingi laki moja na Elfu ishirini (120,000) ifikipo March 01, 2025.

Sauti ya mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Nyihogo, Idd Mitimingi akizungumzia hatua ya kuifukuza SAMBA MICROFINANCE

Kwa upande wake Fatuma Idd amesema kuwa alikopa shilingi laki moja lakini kwa mujibu wa kampuni hiyo ilikata shilingi Elfu kumi na yeye alikabidhiwa shilingi Elfu tisini hivyo katika marejesho yake alitakiwa kurejesha shilingi laki moja na Elfu ishirini march 01, 2025.

Amesema ilipofika Februari 25, 2025 alipeleka rejesho lake kwenye ofisi hiyo ya SAMBA MICROFINACE ili kuepuka riba lakini alivyofika aliambiwa kuwa alipaswa kila siku kurejesha shilingi Elfu nne hivyo anadaiwa shilingi laki mbili na Elfu arobaini.

Nae Khadija Ramadhan amesema alikopa shilingi Elfu themanini na Elfu kumi ilikatwa na kukabidhiwa shilingi Elfu sabini na kutakiwa kurejesha shilingi laki moja lakini aliporejesha Februari 25, 2025 alikataliwa na kudaiwa kuwa anapaswa kulipa shilingi laki moja na Elfu sitini kwani kila siku alipaswa kufanya marejesho ya shilinigi Elfu nne.

Sauti ya akina mama waliokopa SAMBA MICROFINANCE wakielezea maelewano yao kabla ya kukopa na kurejesha fedha za mkopo

Kwa upande wake meneja wa kampuni hiyo John Kambarage ambaye alikataa kurekodiwa sauti yake amesema kuwa vibali vya kufanya kazi ya ukopeshaji wa wananchi wanayo hivyo wapo kisheria na wanafanya kazi hiyo kwa kuzingatia matakwa ya kisheria.

Kampuni ya SAMBA MICROFINANCE imeshikilia mali mbalimbali za akina mama hao wawili ikiwemo TV na Godoro.