Huheso FM
Huheso FM
February 24, 2025, 2:25 pm

“Ulinzi wa miundombinu ya umeme ni jukumu letu sote, toeni taarifa kuhusu wanaohujumu. Pia wananchi epukeni kusogea kwenye Transfoma na njia za umeme kwani ni hatari. Ukiangalia hata hapa kwenye hii Transfoma kuna onyo kabisa kwamba ni HATARI”,amesema Mhandisi Tarimo.
Kijana aliyejulikana kwa jina la Daniel Mageni (27) mkazi wa Kitangili Manispaa ya Shinyanga amefariki kwa kukosa hewa baada ya kupigwa na shoti ya umeme wakati akijaribu kuiba nyaya katika Transfoma iliyopo kitongoji cha Isenegeja Kijiji cha Isela kata ya Samuye.
Mashuhuda wanasema Daniel ambaye ni Fundi Umeme, amekutwa amefariki katika Transfoma iliyopo jirani na Zahanati ya Isela kata ya Samuye Februari 24 mwaka huu huku baiskeli aliyotumia kusafiria na vifaa alivyokuwa akivitumia kukata nyaya vikiwa eneo la tukio.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Isegeneja, Amina Hamis Bwire amesema mwanaume huyo amebainika kupoteza maisha majira ya saa 12 asubuhi baada ya kupigwa na shoti ya umeme wakati akijaribu kujuhumu miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Mhandisi Mwandamizi wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, Anthony Tarimo akizungumza kwa niaba ya Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga amesema kijana huyo amefariki wakati akiingilia njia ya umeme mkubwa katika Transfoma hiyo.
Mhandisi Tarimo amewataka wananchi kuwa waangalifu na kuacha vitendo vya kuhujumu miundombinu ya umeme, akisisitiza kuwa ulinzi wa miundombinu hiyo ni jukumu la kila mmoja. Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo mwananchi huyo amefariki dunia kwa kupigwa na shoti ya umeme wakati akijaribu kuiba waya wa Copper uliokuwa kwenye Transfoma.