Huheso FM

Watumishi watatu CRDB na raia wanne wakamatwa kwa wizi milioni 305 Kahama

July 6, 2024, 4:39 pm

Picha ya eneo la tukio na gari la polisi lililofika kuwachukua watuhumiwa katika tawi la benki ya CRDB Kahama

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawashikilia watu saba, akiwemo meneja huduma kwa wateja na watumishi wengine wawili wa benki ya CRDB tawi la Kahama, kwa tuhuma za wizi wa fedha kiasi cha shilingi milioni 305.

Na Neema Nkumbi-Huheso FM

Kaimu Kamanda wa jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Kenedy Mgani amesema kuwa tukio hilo limetokea  Julai 04, ambapo watu wanne wakazi wa Dar es Salaam walifika katika benki hiyo wakiwa na gari dogo aina ya IST na mwanamke mmoja  alishuka na kuelekea kwa meneja huduma kwa wateja ambapo meneja huyo alimkabidhi  kwa muhudumu wa benki ili aweze kuhudumiwa kama wateja wengine.

Kamanda Mgani amesema mwanamke huyo alimhudumiwa kwa  kupewa fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni 30 kwa kutumia kadi bandia pia alitaka kiasi cha shilingi milioni 275 kuwekwa katika akaunti zingine mbili toafuti katika benki hiyo.

Amesema jeshi hilo lilipata taarifa za siri kuhusiana na wizi huo na kuweka mtego wa haraka na kufanikiwa kuwakamata watu hao wakiwa na fedha taslimu milioni 30 huku fedha zingine zikifungiwa zisiende katika akaunti hizo wakati wenzake wakimsubiri nje kwenye gari lao.

Sauti ya Kaimu kamanda jeshi la polisi mkoani Shinyanga, Kenedy Mgani akielezea undani wa tukio

Kamanda Mgani amesema uchunguzi unaendelea ili kubaini mtandao mzima jinsi gani walijipanga mpaka kutaka kuchukua fedha kupitia akaunti ya mtu bila ridhaa ya mtu kwa kutumia nyaraka  na vitambulisho vya kugushi sambamba na sahihi.