Mgogoro wa miaka 25 soko la Magwanji Kahama watatuliwa
May 16, 2024, 6:09 pm
Na Neema Nkumbi- Huheso Fm
Wakazi wa Mtaa wa Nyakato, Kata ya Nyasubi katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, wameishukuru serikali ya Mtaa huo, kwa kumaliza mgogoro wa soko la Magwanji uliodumu kwa Zaidi ya miaka 25 uliokuwa ukikwamisha kuanza kwa shughuli za soko, sambamba na kuchelewesha maendeleo ya Mtaa.
Wakazi hao ambao ni wajasiriamali, Lulu Shigongo na Flora Peter wakizungumza mara baada ya kumalizika kwa hafla ya uzinduzi wa soko hilo, wamewaomba viongozi wa ngazi za Kata na mitaa, kutoingiza tofauti zao za kisiasa katika miradi ya maendeleo, kwani kufanya hivyo ni kukwamisha maendeleo ya maeneo husika, na kwamba uwepo wa soko hilo utawanufaisha wao binafsi pamoja na kuchangia maendeleo ya mtaa wa Nyakato.
“Ni soko ambalo nalitegemea litakuwa ni kubwa na watu wengi, kwa hiyo pia nimeona nitoke kule nije huku ili pia nipunguze gharamaya nauli, maana mwanzo kwenda kule soko kubwa nilitumia nauli shilingi 2000 kwa siku, lakini hapa sitakuwa na nauli yoyote nitatembea tu, kwa hiyo naishukuru sana serikali” Alisema Flora
Hussein Mwita ni mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakato amewataka wajasiriamali waliopata maeneo katika soko hilo, kuyatumia kama ilivyo makubaliano vinginevyo watapokonywa na kugawiwa kwa watu wengine.
Soko la Magwanji lilikuwa na mvutano wa takribani miaka 25, unaotajwa kukwamisha shughuli za soko pamoja na maendeleo ya mtaa wa Nyakato, limezinduliwa kuanza shughuli zake, linatarajiwa kuwa na wafanyabiashara ndogondogo (machinga) Zaidi ya 300.