Huheso FM

Miundombinu ya umeme yaanza kuwekwa mashine za mpunga Kahama

May 14, 2024, 3:58 pm

Mafundi wa shirika la umeme nchini Tanesco Manispaa ya Kahama wakiweka miundombinu ya umeme maeneo ya mashine za Mpunga kata ya Kagongwa

Siku chache baada ya kurusha taarifa ya changamoto ya kukosekana kwa umeme wa kutosha katika eneo la viwanda vidogo na vya kati vya kuchakata mpunga/mchele, lililopo kata ya Kagongwa manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, shirika la Umeme Tanzania TANESCO wilayani Kahama limeanza kuchukua hatua za kukabiliana na adha hiyo.

Akizungumzia hatua hiyo, meneja wa shirika la ugavi wa umeme Tanzania – TANESCO wilayani Kahama Tumaini Chonya amesema, kinachofanyika ni matengenezo kinga ili kuimarisha upatikanaji wa umeme Kagongwa ikiwemo na maeneo ya mashineni.

“Kwa hiyo leo tunaboresha umeme, kwa kutengeneza matengenezo kinga, na kubadilisha nguzo zote hizi za miti ziwe nguzo za zege ili kuimarisha line yetu na kuimarisha upatikanaji wa umeme katika mji wetu wa Kagongwa” Alisema Chonya

“Mji wetu wa Kagongwa tunaupa kipaumbele kwa sababu ni mji pekee ambao una biashara kubwa una mshine nyingi, na viwanda vingi vya kusindika mpunga, kwa hiyo ndio maana tunaupa kipaumbele cha kutosha, yaani katika wilaya nzima hii ya Kahama, sehem pekee yenye Transformer kubwa ni Kagongwa” Aliongeza Chonya

Nao baadhi ya wafanyabiashara wa Kagongwa waliozungumza na wanahabari akiwemo Dawson Maganyiro wameishukuru TANESCO kwa hatua hiyo, huku Modester Mrema akiiomba serikali kuitazama na miundombinu nyingine katika eneo hilo.

“Niwashukuru sana waandishi wa habari, kuna jambo tuliwaomba mtupelekee serikalini hususan TANESCO, kwa kweli tulikuwa na changamoto ya umeme kukatika kila siku, na wakati mwingine unakuwa singo, lakini tunawashukuru kwa hatua hizi” Alisema Dawson

“Hizi hatua mimi nimefurahi pia, kama nyinyi wanahabari mmetufikia na mkapeleka kero zetu, nilisema siku nikiwaona wanahabari nitasema nao, maana nanyi Mungu amewapa hii kazi muitumikie jamii, si kazi nyepesi” Alisema Modester

Hivi karibuni wafanyabiashara hawa, walitoa kilio chao juu ya changamoto ya umeme kwenye maeneo yao ya biashara, ambapo baada ya siku kadhaa, tayari yameanza kufanyiwa kazi na mamlaka husika ambayo ni TANESCO, hali ambayo imeleta faraja kwao ambapo awali walikata tamaa na kuhisi wamesahaulika licha ya Halmashauri ya manispaa ya Kahama kukusanya mapato makubwa kutoka kwao.