Wanafunzi wapatiwa elimu ya mlipa kodi na TRA
May 10, 2024, 6:38 pm
“Mafunzo ambayo tunayaandaa yanalenga kuwafundisha vijana wetu wakiwa wadogo hasa wanafunzi wa shule za Msingi, Sekondari na vyuoni kujua maana ya kulipa kodi, umuhimu wa kodi ni nini, kwanini serikali zote duniani zinaweka kodi. Kodi ni malipo ya lazima ambayo mwananchi mzalendo anatozwa kwa ajili ya kuisaidia serikali yake iweze kuendesha majukumu yake kwa wananchi”
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga imetoa elimu ya Kodi kwa Wanafunzi wanachama wa Vilabu vya Kodi kutoka shule za Msingi, Sekondari na Vyuo Mkoa wa Shinyanga ili kuwajengea uwezo na ufahamu wa masuala mbalimbali ya kodi.
Mafunzo hayo yamefanyika leo Ijumaa Mei 10,2024 katika Ukumbi wa Makindo Hotel Mjini Shinyanga yakishirikisha wanafunzi kutoka shule ya Msingi Little Treasures, Shule za Sekondari Old Shinyanga, Uhuru na Chuo cha Ualimu Shinyanga (Shy Com) na Chuo cha St. Joseph.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Makwabe David amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea ufahamu wanafunzi kuhusu masuala mbalimbali ya kodi.