Viongozi kituo cha mabasi Kahama wadaiwa kujinufaisha milioni 19, DC Mhita awaka
March 21, 2024, 12:38 pm
Umoja wa vikundi mbalimbali vilivyopo kituo cha mabasi cha CDT wamemuomba mkuu wa Wilaya ya Kahama Mheshimiwa Mboni Mhita kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili katika eneo hilo ikiwemo urejeshwaji wa fedha zinazodaiwa “kutafunwa” na baadhi ya viongozi waliotoka madarakani.
Na Neema Nkumbi-Huheso FM
Hayo yamesomwa katika risala yao iliyosomwa na Shukuru Peter, mbele ya mkuu wa wilaya, Mboni Mhita March 20, 2024 kwenye mkutano ulioandaliwa na wananchi mbalimbali wanaofanya shughuli katika eneo hilo.
Katika risala hiyo wamebainisha changamoto kuwa baadhi ya viongozi waliotoka madarakani wa kituo hicho cha mabasi yaendayo maeneo tofauti katika Wilaya ya Kahama na nje ya Kahama kuwa viongozi hao walijibinafsisha fedha kiasi cha shilingi milioni 19.8 ambazo ni fedha za umoja wa vikundi zilizopatikana kutokana na ada za uanachama, ulinzi na faini.
Pia wananchi hao wameomba kuwezeshwa mikopo ya gharama nafuu ili waweze kujikwamua kiuchumi sambamba na hilo wameomba kituo hicho kufungwa taa ili waweze kufanya kazi usiku na mchana.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita amewaahidi kutatua changamoto hizo na kumtaka kamanda wa jeshi la Polisi Wilaya ya Kahama (OCD) kuwafuatilia waliochukua fedha ili waweze kurudisha na ametoa wiki moja waitwe wasema watalipa hizo fedha kwa namna gani.
Aidha DC Mboni Mhita amewataka akina mama kufanya kazi kwa bidii kuliko kusubiri kuletewa kwani fursa ziko nyingi mfano katika sekta ya madini kuna wawekezaji wengi wanaohitaji kuwekeza hivyo watumie fursa hiyo kuuza vitu mbalimbali ili kujikwamua kiuchumi.