Mechi ya pongezi kwa Taifa Stars yapigwa Kilago, Mgeja asifu vipaji
September 13, 2023, 11:07 pm
Katika mchezo huo Khamis Mgeja amehudhuria kama mgeni rasmi ambapo amepongeza jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuunga mkono na kusapoti michezo na kuwapatia taifa stars milioni mia tano kwa kufanikiwa kufuzu Afcon mwakani 2024 nchini Ivory Coast.
Na Paschal Malulu-Kahama
Mchezo wa kirafiki wa mpira wa miguu kati ya timu ya Nyanhembe Fc dhidi ya Ngudu Fc umemalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1 mchezo uliokuwa maalum kuipongeza timu ya taifa ya Tanzania “Taifa Stars”.
Mechi hiyo iliyoandaliwa na mdau wa michezo Mnyama Nzumbi mkazi wa Kijiji cha Nyanhembe umepigwa Septemba 13, 2023 ulikuwa maalum kuipongeza timu ya taifa ya Tanzania kwa kufuzu michuano ya mataifa ya Africa”Afcon” kwa mara ya tatu ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1980, 2019 na 2023.
Katika mchezo huo mgeni rasmi alikuwa mwenyekiti mstaafu wa chama cha soka mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) Khamis Mgeja ambaye amesifu ushindani uliooneshwa na timu zote mbili Nyanhembe Fc na Ngudu Fc na kupelekea kutoka sare ya bao moja kwa moja.
Mgeja amesema kuwa hivi sasa vipaji vingi kwenye mpira wa miguu vipo vijijini hivyo kuviomba vilabu ambavyo vina uwezo wa kusajili wachezaji vitembelee vijijini na kuona vipaji vilivyoko huko na kuvikuza ili kutunza hazina ya taifa.
Mbali na hilo Khamis Mgeja amempongeza Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuunga mkono michezo nchini akitolea mfano kuipatia Taifa Stars milioni mia tano “500” akisema kuwa hiyo ni chachu mkwa vijana ili kuwatia moyo wa kulitetea taifa. Aidha Mgeja amewaomba wadau na makampuni mbalimbali kumuunga mkono Mhe. Rais kwa kile anachokifanya kwenye michezo nao waguswe kuwekeza ili kuukuza zaidi na kuwa katika ushindani wa kimataifa zaidi.